Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 July 2026, 13:24

Na Elias Maganga
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amesimamia utatuzi wa migogoro miwili ya ardhi katika Kijiji cha Michenga, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, iliyokuwa imedumu kwa miaka kadhaa na kufikishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kilombero.
Akisoma hukumu zilizotolewa na Baraza la Ardhi na Nyumba, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa katika kesi iliyowahusisha Yusuph Faya na Ibrahim Faya dhidi ya Fatuma Ululuti, iliyofunguliwa mwaka 2018, hukumu iliyotolewa tarehe 29 Septemba 2023 imewatambua Ibrahim Faya na Yusuph Faya kuwa wamiliki halali wa shamba lenye ukubwa wa ekari tisa.

Katika mgogoro mwingine uliomhusisha Clencesia Bilingi dhidi ya Khadija Baraza, Mkuu wa Wilaya amesema Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kilombero/Malinyi limetoa hukumu inayomtambua Khadija Baraza kuwa mmiliki halali wa eneo lililokuwa likigombaniwa.
Kutokana na hukumu hizo, Mkuu wa Wilaya, Wakili Dunstan Kyobya, amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha wiki mbili, wataalamu wa ardhi wanafika katika Kijiji cha Michenga kwa ajili ya kupima shamba lenye ukubwa wa ekari tisa na kuwakabidhi rasmi wamiliki halali, Ibrahim Faya na Yusuph Faya.
Aidha, utatuzi wa migogoro hiyo umefanyika moja kwa moja katika maeneo husika mbele ya wahusika na mashahidi, hatua iliyowezesha pande zote kuona mipaka na kuthibitisha maeneo yanayohusika.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Michenga akiwemo Imelda Medard Mwamuheni wamepongeza hatua ya Mkuu wa Wilaya kufika mwenyewe katika maeneo yenye migogoro na kusimamia utekelezaji wa hukumu, wakisema hatua hiyo imeondoa taharuki na kurejesha amani ambayo walikuwa wameikosa kwa muda mrefu.
