Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
31 August 2026, 21:03

Shule ya Msingi Ihowanja wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, imepata madarasa mawili mapya pamoja na madawati 30 kupitia Vodacom Tanzania Foundation, hatua inayolenga kupunguza uhaba wa madarasa uliokuwa ukiifikia 16 na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi.
Na: Latipha Twaleb
Vodacom Tanzania kupitia Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi madarasa mawili mapya pamoja na madawati 30 kwa Shule ya Msingi Ihowanja, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Msaada huo unatarajiwa kuongeza nafasi za kujifunzia na kupunguza changamoto ya miundombinu iliyokuwa ikiikabili shule hiyo, huku ukilenga pia kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania PLC, Chiha Nchimbi, amesema ujenzi wa madarasa hayo ni sehemu ya mpango wa kampuni hiyo wa kushirikiana na jamii kuboresha mazingira ya elimu, hususan kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihowanja, Iddy Mgonja, ameishukuru Vodacom Tanzania kwa kujenga madarasa mawili mapya na kutoa madawati 30, akisema kabla ya ujenzi huo shule ilikuwa ikikabiliwa na uhaba wa madarasa 16. Amesema hatua hiyo imepunguza changamoto ya miundombinu ya kujifunzia na kutoa mazingira bora zaidi kwa wanafunzi na walimu.

Naye Diwani wa Kata ya Kilosampepo, Boniventure Killian Mwanga, amepongeza hatua hiyo, akisema ushirikiano kati ya sekta binafsi, Serikali na jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira salama na rafiki ya kujifunzia.