Pambazuko FM Radio

Agricom yapeleka zana Mlenge

10 August 2026, 11:32

Mkuu wa wilaya ya Iringa B. Sitta akisaini kitabu cha wageni banda la Agricom – picha na; Madaraka Mdesa

Kampuni ya Agricom Tawi la Ifakara imepeleka zana za kilimo katika Kata ya Mlenge, Tarafa ya Pawaga mkoani Iringa, kuwawezesha wakulima kupata zana za kisasa na kuwaunganisha na taasisi za kifedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo hiyo.

Na: Isidory Mtunda

Kampuni ya zana za kilimo ya Agricom, Tawi la Ifakara, imepeleka mitambo ya kilimo katika Kata ya Mlenge, Tarafa ya Pawaga mkoani Iringa, ambako kampuni hiyo haina tawi, kwa lengo la kuwafikia wakulima na kuwahamasisha kutumia zana za kisasa ili kurahisisha na kuboresha shughuli za kilimo.

Afisa mauzo Madaraka (mwenye T-shirt nyeupe) akiwa na wateja wa Pawa tiller – picha na; Madaraka Mdesa

Akizungumza na Pambazuko FM katika viwanja vya maonesho ya Nane Nane Kata ya Mlenge, Afisa Mauzo wa Agricom Ifakara, Madaraka Mdesa, amesema kampuni hiyo imepeleka mitambo mbalimbali ya kilimo kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza ufanisi katika uzalishaji. Amesema Agricom pia inawaunganisha wakulima na taasisi za kifedha, ikiwemo benki, ili kuwawezesha kupata mitaji ya kununua zana hizo.

Sauti ya Madaraka Mdesa

Kwa upande wake mheshimiwa  Diwani wa Kata ya Mlenge, Tarafa ya Pawaga; Fundi Ahmadi Mihayo amesema maonesho ya Nane Nane yanayofanyika ngazi ya kata yanalenga kuwafikishia wananchi elimu na fursa za kiuchumi, ikiwemo matumizi ya zana bora za kilimo na kuwaunganisha wakulima wadogo na taasisi za kifedha. Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa baadhi ya wakulima hawawezi kusafiri hadi kwenye maonesho ya kikanda yanayofanyika mkoani Mbeya.

Sauti ya Mh. Diwani Mihayo

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa na mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho hayo, Benjamin Samweli Sitta, amepongeza mwitikio wa wakazi wa Kata ya Mlenge katika kununua mashine za kilimo, ikiwemo power tiller zilizopelekwa na Agricom Tawi la Ifakara. Amesema matumizi ya zana hizo yatasaidia kurahisisha shughuli za kilimo na kuongeza ufanisi wa wakulima.

DC Benjamini Sita (mwenye suti nyeusi)alipotembelea banda la Agricom Mlenge – picha na; Madaraka Mdesa
Sauti ya DC Benjamini Sitta