Pambazuko FM Radio

Madereva wa matrekta, power tiller waaswa

1 August 2026, 13:10

Wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller wakimsikiliza DTO Blandina Kasongwa. Picha na: WP9079 Mary Bayo

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limewataka madereva wa matrekta na Power Tiller kuzingatia sheria za usalama barabarani, huku likieleza kuwa Power Tiller hairuhusiwi kubeba abiria kwa mujibu wa sheria.

Na: Isidory Mtunda

Madereva wa matrekta na Power Tiller katika tarafa ya Mlimba, Halmashauri ya wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro, wametakiwa kuendesha vyombo vyao barabarani kwa tahadhari kubwa kana kwamba wanaendesha vyombo vitatu kwa wakati mmoja, ili kupunguza ajali za barabarani.

Wito huo umetolewa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa Kata ya Chisano, A/Insp. Nassoro Mwinyi, wakati wa mafunzo kwa wamiliki na madereva wa matrekta na Power Tiller yaliyofanyika katika Kituo cha Polisi Mlimba na kuratibiwa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani (DTO) Wilaya ya Kilombero, ASP Blandina Benedict Kasongwa.

Sauti ya A/Insp. Nassoro Mwinyi

Kwa upande wake, ASP Blandina Kasongwa amewataka askari wa usalama barabarani kuacha kuwafukuza madereva wanaokwepa kusimama wanaposimamishwa, akieleza kuwa ni salama zaidi kuwafuatilia na kuwakamata baadaye majumbani au maeneo wanayofahamika, badala ya kuhatarisha maisha kwa kufukuzana nao barabarani.

ASP Blandina Kasongwa akionesha kifaa cha kupima kilevi kwa madereva. Picha na: WP9079 Mary Bayo
Sauti ya ASP B. Kasongwa

Baada ya mafunzo hayo, washiriki waliuliza maswali kuhusu utaratibu wa kupata leseni za udereva wa matrekta, usajili wa matrekta na matela yake, gharama za mafunzo, upatikanaji wa mafundi wa mifumo ya umeme wa matrekta, pamoja na idadi ya watu wanaoruhusiwa kubebwa kwenye Power Tiller

Sauti za wananchi

Akijibu maswali hayo, ASP Kasongwa alisema Jeshi la Polisi litashirikiana na wataalamu wa umeme wa magari pamoja na TBS kutatua changamoto za usajili, na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, Power Tiller hairuhusiwi kubeba abiria, bali inapaswa kusafirishwa kama ilivyo kwa mashine za kilimo aina ya Combine Harvester.