Pambazuko FM Radio

UKICU yapokea mizani kidigitali 70

14 May 2026, 12:50

Mzani wa kidigitali – picha na: Katalina Liombechi

Chama Kikuu cha Ushirika Ulanga Kilombero (UKICU) kimepokea mizani 70 za kidigitali kutoka kampuni ya ROTAI kwa lengo la kuboresha usahihi wa vipimo vya mazao na kuongeza uwazi kwa wakulima kupitia mfumo wa kidigitali unaotuma taarifa moja kwa moja kwenye simu za mkulima.

Na: Isidory Mtunda

Chama Kikuu cha Ushirika Ulanga Kilombero (UKICU) kimepokea mizani 70 za kidigitali kutoka kampuni ya ROTAI kwa ajili ya kusaidia vyama vya msingi na AMCOS kutatua changamoto ya vipimo visivyo sahihi vya mazao. Mfumo huo unatarajiwa kumpatia mkulima taarifa kamili za mzigo wake ikiwemo idadi ya kilo, bei pamoja na risiti kupitia ujumbe mfupi wa simu mara baada ya mazao kupimwa. Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero uliopo Kibaoni, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni ya ROTAI Ltd, Gidion David amesema mfumo huo wa kidigitali utasaidia kuongeza uwazi, kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za vyama vya ushirika na kurahisisha ufuatiliaji wa taarifa kwa serikali na wakulima.

Bwana Gidion David – picha na: Katalina Liombechi
sauti ya Gidion David kutoka Rotai

Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rosalia Rwegasira amesema mizani hiyo ni mkombozi kwa wakulima kwani itaondoa matumizi ya vipimo visivyo sahihi vinavyotumiwa na baadhi ya wanunuzi. Amesisitiza viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia matumizi sahihi ya mizani hiyo ili kuhakikisha wakulima wanapata haki yao.

Dkt. Rosalia Rwegasira – katibu tawala msaidizi – picha na; Katalina Liombechi
sauti ya Dr. Rosalia

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kilosa Mpepo AMCOS na mjumbe wa UKICU, Ritha Nyela amesema ujio wa mizani hiyo utasaidia wakulima kupata vipimo sahihi na kuongeza imani katika mfumo wa ushirika. Aidha amesema changamoto zozote za kiufundi zitashughulikiwa kwa ushirikiano na kampuni ya ROTAI.

sauti ya Ritha Nyela

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Wakili Sebastiani Wariuba amewataka viongozi wa vyama vya msingi kuwa waadilifu na kutumia mizani hiyo kwa weledi, akionya kuwa teknolojia hiyo inaweza kuchakachuliwa au kuharibiwa iwapo hakutakuwa na usimamizi mzuri na uaminifu kutoka kwa watumiaji wake.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Malinyi