Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 July 2026, 18:16

Benki ya CRDB imekabidhi vitanda 33 vya wagonjwa na makabati 26 vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa Hospitali ya Saratani ya Good Samaritan Ifakara, ili kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa.
Na: Hospice Lipipa
Benki ya CRDB imekabidhi vitanda 33 vya wagonjwa pamoja na makabati 26 vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa Hospitali ya Saratani ya Good Samaritan iliyopo Ifakara, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro. Msaada huo unalenga kuboresha huduma za matibabu na kuongeza uwezo wa hospitali kuwahudumia wagonjwa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Admin Mwansasu, amesema msaada huo ni sehemu ya mpango wa benki wa kurejesha kwa jamii asilimia moja ya faida inayopatikana kila mwaka kupitia shughuli zake za biashara. Amesema CRDB itaendelea kutekeleza mpango huo katika maeneo mbalimbali nchini yenye mahitaji ya huduma za afya.

Kwa niaba ya Hospitali ya Good Samaritan, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Shibiri James, amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vitanda na vifaa vingine kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Good Samaritan, Dkt. Rosemary Mushi, amesema hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia vifaa mbalimbali, hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia wagonjwa wengi kupata huduma kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya afya. Amesema pamoja na huduma bora zinazotolewa na Hospitali ya Good Samaritan, mahitaji ya vifaa tiba bado yanaendelea kuongezeka, hivyo ameitaka benki hiyo kuendelea kuisaidia hospitali kupitia programu zake za uwajibikaji kwa jamii.
