Pambazuko FM Radio

TFS Kilombero yatoa madawati 50

24 August 2026, 22:48

TFS Kilombero imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni saba kwa Shule ya Msingi Signal, ikiwa ni sehemu ya kurejesha fadhila kwa wananchi wanaoshiriki katika uhifadhi wa Msitu wa Nangachi. Msaada huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia huku viongozi wakitoa wito wa kuimarisha uhifadhi wa misitu na lishe kwa wanafunzi.

Na: kuruthum Mkata

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero umetoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni saba kwa Shule ya Msingi Signal, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Meneja wa TFS Kilombero, Bi. Zarina Shaweji, amesema msaada huo ni sehemu ya kurejesha fadhila kwa wananchi wanaoshiriki katika uhifadhi wa Msitu wa Nangachi. Amesema TFS inatambua mchango wa wananchi katika kulinda msitu huo, huku akiwataka kuacha shughuli za kibinadamu na uchomaji moto ndani ya msitu.

Zarina Sheweji wakati hafla ya kukabidhi madawati – picha na: Kuruthum Mkata
Sauti ya Zarina Sheweji – Meneja

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mhe. Abubakary Asenga, ameishukuru TFS kwa msaada huo, huku akiitaka taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wananchi na TFS katika maeneo ya hifadhi. Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuendelea kuchangia lishe shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza vizuri na kuongeza ufaulu.

Abubakari Asenga (MB) akitoa neno wakati wa hafla hiyo – picha na: Kuruthum Mkata
Sauti ya Mbunge A. Asenga

Naye Diwani wa Kata ya Signal, Hassan Meza, amesema shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, ambapo madawati 75 yalikuwa yakitumika kuhudumia wanafunzi wapatao 900. Amesema msaada wa madawati 50 kutoka TFS utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati shuleni hapo.

Sauti ya Hasan Meza