Pambazuko FM Radio

Waziri Masauni akemea Uharibifu wa Mto Lumemo Ifakara

30 September 2026, 11:51

Ni marufuku kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji hasa Mto Lumemo ili kuepukana na ukame unaoweza kutokea, ni vyema tukapanda miti-Waziri Masauni

waziri Hamadi Masauni akizungumza na Viongozi mbalimbali kando ya Mto Lumemo Wilayani Kilombero picha na Kuruthum Mkata

Na Kuruthum Mkata

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amekemea vitendo vya uharibifu wa mazingira kando ya Mto Lumemo mjini Ifakara, akisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji kwa maendeleo ya sasa na ya baadaye.

Masauni ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua tuta lililokatika katika eneo la Kiungani, Ifakara ambapo Amesema Mto Lumemo ni eneo la kimkakati, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira badala ya kuyaharibu.

waziri Mhandisi Hamad Masauni akitoa maelekezo kwa Viongozi wa NEMC na Wilaya ya Kilombero kando ya Mto Lumemo Ifakara Picha na Kuruthum Mkata

Aidha, amekemea mifugo kuingizwa katika maeneo ya vyanzo vya maji, akieleza kuwa hali hiyo huchangia uharibifu wa mazingira na kuongeza hatari ya ukame. Pia amewataka viongozi kusimamia hatua za kujikinga na mafuriko yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa.

sauti ya Waziri Masauni

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira kutoka NEMC, Elibariki Bajuta akitoa maelezo Mbele ya Waziri Masauni Picha na Kuruthum Mkata

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira kutoka NEMC, Elibariki Bajuta,Amewataka wananchi kuacha kutupa taka kwenye mito na mitaro, huku likisisitiza umuhimu wa kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji ili kupunguza athari za mazingira.

Bwana Bajuta pia imetoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi mabondeni kuhama maeneo hatarishi mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua.

sauti ya Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira kutoka NEMC, Elibariki Bajuta

Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Kidakio cha Kilombero Abisai Chilunda akitoa maelezo ya Mto Lumemo kwa Waziri wa Mazingira Mhandisi Hamad Masauni picha na Kuruthum Mkata

Naye Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Kidakio cha Kilombero Abisai Chilunda amesema Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa Mto Lumemo, na kwamba kazi za marekebisho ya maeneo yaliyoathirika zinatarajiwa kuanza ndani ya wiki hii.

sauti ya Afisa wa Maji Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Kidakio cha Kilombero Abisai Chilunda