Pambazuko FM Radio

DC Kyobya aagiza Watumishi wa Afya wapelekwe Utengule, Mlimba.

6 November 2026, 15:09

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Wakili Dunstan Kyobya ikikagua Jengo la Zahanati ya Utengule Halmashauri ya Mlimba Picha na Kuruthum Mkata

Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lililokamilika lianze kutoa Huduma na Mkurugenzi shughulikia hili haraka iwezekanavyo wakati mnaendelea na Ujenzi wa Majengo mengine -DC Kyobya.

NanKuruthum Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kupeleka watumishi wa afya katika Kituo cha Afya Utengule kabla ya kukamilika kwa ujenzi wake.

Amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kuanza kupata huduma za awali za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Wakili Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero akitoa maagizo juu ya Zahanati ya Utengule picha na Kuruthum Mkata

Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, ambapo amewapongeza kwa hatua iliyofikiwa.

sauti ya DC Kyobya

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Dkt. Dorothy Maganga akiisikiliza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero picha na Kuruthum Mkata

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Dkt. Dorothy Maganga, amesema kituo hicho kinahitaji kukamilishwa kwa majengo matatu muhimu.

Majengo hayo ni OPD, maabara na wodi ya kulaza wagonjwa. Hadi sasa, jengo la OPD pekee ndilo limekamilika.

sauti ya Kaimu DMO

Diwani wa Kata ya Utengule, Anthony Mnyagani, akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero

Naye Diwani wa Kata ya Utengule, Anthony Mnyagani, amesema wananchi wanakabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, huku kituo hicho pia kikikabiliwa na ukosefu wa maji.

Ameiomba Serikali kuhakikisha ujenzi wa majengo yaliyosalia unakamilishwa pamoja na kutatua changamoto ya maji ili wananchi wapate huduma bora za afya karibu na makazi yao.

sauti ya Diwani Anthony

Mwenyekiti wa Kijiji cha Utengule, Thomas Mashangila, akizungumza mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero picha na Kuruthum Mkata

Mwenyekiti wa Kijiji cha Utengule, Thomas Mashangila, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwa kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu.

Ameiomba Serikali na wadau wengine kuongeza nguvu katika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ili kianze kutoa huduma zote zilizokusudiwa.