Pambazuko FM Radio

Siku 30 zatosha kutatua Mgogoro uliodumu kwa Miaka 17 Chikago Ifakara?

20 November 2026, 15:06

Baadhi ya Maofisa Ardhi wa Halmashauri ya Miji wa Ifakara wakisimama mbele ya Wananchi wa Kijiji cha Chikago Kidatu Ifakara picha na Kuruthum Mkata

suala hili limekaa muda mrefu nawapa siku thelathini kulishughulikia na kulimaliza-DC Kilombero

Na Kuruthum Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ameipa Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara mwezi mmoja kukamilisha upimaji wa maeneo yaliyotengwa kwa wananchi waliopisha eneo la shule Chicago, Kata ya Kidatu, ili kumaliza mgogoro wa ardhi wa miaka 17.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kitongoji cha Mlabani, Kyobya amesema kati ya wananchi 20 walioathiriwa na mgogoro huo, 17 wamekubali kupatiwa maeneo mbadala, huku watatu wakiwa hawajakamilisha makubaliano.

Amewashauri wananchi hao kukamilisha taratibu za kufungua mirathi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda haki zao hadi watakapopatiwa maeneo waliyotengewa.

Wakili Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero icha na Kuruthum Mkata

sauti ya DC Kyobya

Kwa upande wake,Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Mji wa Ifakara amesema watahakikisha zoezi la upimaji linafanyika kwa kushirikiana na wananchi ili kuondoa migogoro ya ardhi, huku wakipanga kuunda kamati zitakazosaidia kusimamia maeneo hayo. Pia amewataka wananchi kuacha kuuza maeneo ya Serikali.

sauti ya Mkuu wa Idara ya Ardhi Ifakara Mji

Naye Diwani wa Kata ya Kidatu Fransisi Matangula amesema mgogoro huo umekuwa changamoto kwa wananchi na kuiomba Serikali kuhakikisha unatatuliwa ili kurejesha utulivu katika eneo hilo.

Diwani wa Kata ya Kidati Fransis Matangula akizungumza katika kikao hicho picha na Kuruthum Mkata

Akielezea historia ya mgogoro huo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlabani, Raymond Mbumi, amesema wananchi walifikia makubaliano ya kugawiwa maeneo mengine, ambapo 17 kati ya 20 walikubali utaratibu huo.

sauti ya Mwenyekiti

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaodai kuwa na maeneo katika eneo hilo, akiwemo Kassim Angani, wamesema wanahitaji fidia kwa madai kuwa eneo hilo lilikuwa mali ya wananchi kwa muda mrefu na si eneo la shule, huku wakieleza kuwa wamesimamishwa kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo hayo.