Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
17 November 2026, 19:38

Kuna baadhi ya watu wanaingia kwa vibali halali lakini wanavuka muda wa kukaa bado tunawaita wahamiaji haramu wanatakiwa waripotiwe
Na Katalina Liombechi
Jamii imetakiwa kuwa makini na wageni wanaoingia na kuishi katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanawatambua na kuwaripoti kwa mamlaka husika ili kudhibiti wahamiaji haramu na kulinda usalama wa nchi.
Wito huo umetolewa Novemba 17, 2026, na Mrakibu wa Uhamiaji Wilaya ya Kilombero Emily Mwakyusa, akizungumza na Pambazuko FM ofisini kwake, ambapo amesema kumekuwa na uwepo wa baadhi ya wageni wanaoingia nchini kwa vibali halali wamekuwa wakivuka muda wa vibali vyao na hivyo inatafsirika kuwa wanaishi nchini pasi ya kuwa na uhalali.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa za wageni wanaowapokea ili kuwezesha mamlaka kufuatilia mienendo yao na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Magengeni, Kata ya Viwanja Sitini, Peter Tweve, amesema licha ya kutoa elimu kupitia mikutano ya wananchi, bado mwitikio wa wakazi kuripoti wageni wanaoingia katika maeneo yao ni mdogo, hali inayoweza kuhatarisha usalama.

Aidha, Mrakibu wa Uhamiaji Amesema Idara hiyo imekuwa ikiendesha kampeni ya Mjue Jirani Yako pamoja na kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uhamiaji na wajibu wao katika kulinda usalama wa nchi huku akielezea kazi zinazofanywa na idara.