Pambazuko FM Radio

Kamati za Mazingira zajengewa Uwezo Kando ya Miteremko ya Uzungwa

12 November 2026, 11:56

Baadhi ya Washiriki wa Kamati za Mazingira kutoka Vijiji nane wakijengewa Uwezo picha na Hifadhi ya Mazingira Asili Uzungwa Scarp

Lengo ni kuzijengea uwezo kamati hizo ili ili ziwe na ufanisi katika majukumu yao kwa ushirikiano na jamii katika kulinda rasilimali za asili -Mhifadhi Maiko Urio

Na Katalina Liombechi

Kamati za mazingira kutoka vijiji nane vinavyozunguka hifadhi ya Mazingira Asili Uzungwa Scarp inayosimamiwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS, wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kuimarisha uwezo wao katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya uhifadhi wa misitu, mazingira na vyanzo vya maji.

Vijiji vilivyonufaika na mafunzo hayo ni Udagaji, Lufulu, Chinganda, Chita, Makutano, Ikule, Kidete na Itongoa.

washiriki wakifundishwa Viambata vya Utawala Bora Picha na Hifadhi ya Mazingira Asili Uzungwa Scarp

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Mhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Hifadhi ya Mazingira Asili ya Uzungwa Scarp, Maiko Urio, amesema lengo ni kuzijengea uwezo kamati hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuendelea kushirikiana na jamii katika kulinda rasilimali za asili.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi katika kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa Hifadhi ya Mazingira Asili ya Uzungwa Scarp.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Mfuko wa Kuhifadhi Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) na yamefanyika kwa muda wa siku tano, kuanzia Novemba 7 hadi 11, 2026.

Sauti ya Mhifadhi