Pambazuko FM Radio

TAWA yapanda miti 2,500 hifadhi Utengule

16 April 2026, 3:25 pm

Afisa tarafa Mlimba na wahifadhi wa TAWA wakipanda mche wa mti – picha na; Isidory Mtunda

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA,  inaendelea na juhudi za kurejesha uoto wa asili katika Hifadhi ya Kilombero ‘ Eneo A’ kwa kupanda miche ya miti 2,500, huku ikiimarisha ulinzi wa eneo hilo na kushirikisha jamii katika uhifadhi wa mazingira.

Na; Isidory Mtunda

TAWA imeendesha zoezi la upandaji wa miche ya miti 2,500 katika eneo la hekta 30 ndani ya Hifadhi ya Kilombero ‘A’, eneo la Utengule, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uoto wa asili uliokuwa umeharibika.

Kamanda Kagoma akipanda mti – picha na; Isidory Mtunda

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mhifadhi mkuu wa Hifadhi ya Wanyamapori Kilombero, Bigilamungu Kagoma, amesema shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na ujenzi wa makazi zimesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuacha maeneo mengi wazi.

Sauti ya kamanda Kagoma 1

Aidha, Kagoma ameushukuru mradi wa Food Systems, Land Use and Restoration Program – FOLUR kwa kuunga mkono juhudi za urejeshaji wa mazingira, akieleza kuwa mradi huo unasaidia kufanikisha malengo ya kurejesha maeneo yaliyoharibiwa katika hali yake ya asili.

Sauti ya kamanda Kagoma 2

Kwa upande wake, Mhifadhi mwandamizi na msimamizi wa Hifadhi ya Kilombero ‘A’, Bedui Mboto, amesema kutokana na changamoto za uharibifu unaojirudia, TAWA imeanza kujenga kituo kidogo cha askari (Ranger post) ili kuimarisha ulinzi wa hifadhi hiyo.

Mhifadhi mwandamizi hifadhi ya Kilombero ‘A’ kamanda Mboto – picha na; Isidory Mtunda

Ameongeza kuwa mwezi Agosti mwaka jana, baadhi ya wananchi waliharibu miundombinu ya hifadhi kwa kung’oa alama za mipaka (beacons) 36 zenye thamani ya takribani shilingi milioni saba na kuchoma moto vifaa vya mkandarasi aliyekuwa akijenga kituo hicho.

sauti ya kamanda Mboto

Naye Mtendaji wa Kijiji cha Utengule, Hassan Omary Pamuhi, ameishukuru TAWA kwa juhudi hizo za upandaji miti, akisema zitasaidia kurejesha uoto wa asili na kuboresha mazingira ya eneo hilo. Ameahidi kuwa uongozi wa kijiji utaendelea kushirikiana na taasisi hiyo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Mtendaji wa kijiji cha Utengule- Hassan Pamuhi – picha na; Isidory Mtunda
sauti ya mtendaji kijiji – Utengule – Pamuhi

Juhudi za urejeshaji wa uoto wa asili ni sehemu ya mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi na upotevu wa bioanuai. Miradi kama Food Systems, Land Use and Restoration Program inalenga kusaidia nchi ikiwemo Tanzania kurejesha mifumo ya ikolojia, kuboresha matumizi ya ardhi na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.