Pambazuko FM Radio

 ULS yasaidia Mil 8.95 huduma za Afya Kanyenja

18 June 2026, 19:56

Picha ya Viongozi wa STEP kulia na kushoto ni viongozi wa kijiji cha Kanyenja(Picha na Katalina Liombechi)

Fedha hizo ni kusaidia ujenzi wa jengo la mama na mtotokatika zahanati ya Kijiji Kanyenja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ULS wenye lengo la kujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi wanaopakana na hifadhi zilizopo katika Ushoroba wa wanyamapori wa Udzungwa – Nyerere

Na Katalina Liombechi

Wananchi wa Kijiji cha Kanyenja, Kata ya Mang’ula B, wameonyesha dhamira yao ya kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori baada ya kusaini mkataba wa uhifadhi na kupokea hundi yenye thamani ya shilingi milioni 8.95 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika zahanati ya kijiji hicho.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Mandhari ya Milima ya Udzungwa (Udzungwa Landscape Strategy – ULS), unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) na Mazingira Alliance for Community and Conservation (MACCO)kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya jamii zinazopakana na maeneo ya hifadhi na wadau wa uhifadhi.

Akizungumza hivi karibuni baada ya hafla ya utiaji saini wa mkataba huo na makabidhiano ya hundi, Mkurugenzi wa STEP, Bw. Frank Lihwa, amesema mradi wa ULS ni wa miaka 20 na unafadhiliwa na Hempel Foundation na Aage V. Jensen Charity Foundation.

Ameeleza kuwa mradi huo umebuniwa ili kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya uhifadhi wanapata manufaa ya moja kwa moja kupitia miradi ya maendeleo ya kijamii.

Aidha, amesema huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na maendeleo ya jamii zitaimarishwa kupitia ushirikiano huo.

Picha ya Frank Lihwa Mgurugenzi Mtendaji STEP(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Frank Lihwa Mkurugenzi Mtendaji STEP 1

Naye meneja wa Ushoroba STEP Joseph Mwalugelo amesema kupitia miradi kama hiyo, wananchi wanapata motisha ya kuendelea kushiriki katika shughuli za uhifadhi huku utegemezi mkubwa wa rasilimali zinazotoka ndani ya maeneo ya hifadhi ukipungua.

Sauti ya Joseph Mwalugelo Meneja wa Ushoroba STEP 2

Kwa upande wao, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho pamoja nao wananchi wa Kanjenja wameeleza kufurahishwa na msaada huo, wakisema kuwa fedha hizo zitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wanawake wajawazito, akina mama na watoto katika kijiji hicho.

Walibainisha kuwa mradi huo umeonyesha kwa vitendo jinsi uhifadhi unavyoweza kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

Wananchi hao wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya jamii, serikali na mashirika ya uhifadhi ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii yanaenda sambamba na uhifadhi endelevu wa mazingira na wanyamapori.

Picha ya Viongozi wa STEP kwenye Picha ya Pamoja na wananchi wa Kanyenja baada ya kusaini Mkataba(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Wananchi wa Kanyenja 3
Picha ya Jengo la Zahanati ya Kanyenja ambapo STEP Kupitia ULS itajenga jengo la Mama na Mtoto(Picha na Katalina Liombechi)

Mradi wa Mandhari ya Milima ya Udzungwa unaendelea kuwa mfano wa namna uhifadhi unavyoweza kutumika kama chombo cha maendeleo ya jamii, kwa kuunganisha malengo ya kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi.

Kupitia uwekezaji katika huduma za kijamii, mradi huo unalenga kujenga jamii zenye ustahimilivu, zenye uelewa wa umuhimu wa uhifadhi, na zinazoshiriki kikamilifu katika kulinda urithi wa asili wa Tanzania.