Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
8 May 2026, 12:18

Msaada uliotolewa ni pamoja na vyandarua 59, ndoo 39, mikeka 42, blanketi 88 pamoja na mahindi zaidi ya tani sita
Na Kuruthumu Mkata
Zaidi ya kaya 59 kutoka Kata ya Mngeta Halmashauri ya Mlimba zimeathirika na mafuriko yaliyotokea katika eneo hilo, ambapo Serikali imewapatia msaada wa tani 23 za mahindi pamoja na vifaa mbalimbali muhimu kwa matumizi ya waathirika hao.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Mtendaji wa Kata ya Mngeta Catherine Madeghe wakati akisoma taarifa ya waathirika wa mafuriko mbele ya mkuu wa wilaya ya kilombero wakili dunstan kyobya amesema kuwa jumla ya kaya 59 zenye wakazi zaidi ya 200 zimeathirika na mafuriko hayo akieleza kuwa kupitia msaada huo uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, wananchi wa Kata ya Mngeta wamepokea vyandarua 59, ndoo 39, mikeka 42, blanketi 88 pamoja na mahindi zaidi ya tani sita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, akizungumza Mei 6,2026 akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Serikali amesema Serikali inatambua athari za maafa yaliyotokea katika Halmashauri ya Mlimba na ndiyo sababu imeamua kuwafariji wananchi kwa kutoa misaada hiyo,ambapo pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali waathirika wa maafa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba amesema licha ya umbali wa halmashauri hiyo, Serikali bado imeendelea kusikiliza na kuwafikia wananchi wake kwa misaada na huduma mbalimbali za kimaendeleo ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata msaada wanapokumbwa na changamoto.
Naye Diwani Kata ya Mngeta Andrew Maganjila amesema wananchi wa kata hiyo wanaishukuru Serikali yao pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba kwa kufanya juhudi za kufanikisha upatikanaji wa misaada hiyo kwa wakati.
Baadhi ya waathirika wa mafuriko kutoka Kata ya Mngeta,Baraka Mwakajoka na Sophia Kenani, wameipongeza Serikali pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kilombero kwa kuwafikia na kuwapatia msaada katika kipindi kigumu walichopitia.