Pambazuko FM Radio

Uzungwa Scarp yaendeleza uhifadhi mazingira kupitia FOLUR

14 May 2026, 20:53

Picha ya Wahifadhi na baadhi ya wananchi walioshiriki kupanda miti(Picha kwa hisani ya Uzungwa Scarp)

Mradi wa FOLUR unaendelea kuleta matokeo chanya kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na uzalishaji endelevu

Na Katalina Liombechi

Hifadhi ya Mazingira Asili Uzungwa Scarp imepanda zaidi ya miti elfu nane ya Mikangazi na Mikenge katika safu ya Chita, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshaji wa Mifumo ya Chakula, maarufu FOLUR.

Mradi huo unalenga kurejesha uoto wa asili, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai pamoja na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira.

Mhifadhi daraja la kwanza kutoka hifadhi hiyo, Maiko Urio, amesema mradi huo unaendelea kuleta matokeo chanya kwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na uzalishaji endelevu wa chakula kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine  kupitia Mradi huo wa FOLUR Hifadhi ya Mazingira Asili Uzungwa Scarp pia wametoa mafunzo ya kukabiliana na mioto ya misituni kwa zaidi ya wananchi mia mbili kutoka vijiji vinane vinavyozunguka hifadhi hiyo amnapo kwa Safu ya Chita ni vijiji vya Udagaji,lufulu,Ching’anda,Chita,Makutano,Ikule,Kidete na itongoa.

Sauti ya Mhifadhi Maiko Urio 1

Aidha pamoja na mambo mengine Mhifadhi Maiko ameelezea umuhimu wa hifadhi hiyo kiikolojia na tija iliyopo kwa shughuli za utalii na matumizi mengine endelevu.

Sauti ya Maiko Urio 2

Kwa upande wake miongoni mwa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Arafat Mtui, amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuzuia moto na kushiriki katika kulinda mazingira.

Picha ya Wananchi wakipatiwa mafunzo(Picha kwa hisani ya Uzungwa scarp)

Mioto ya misituni imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa bioanuwai, vyanzo vya maji na makazi ya viumbe mbalimbali. Kupitia mafunzo haya tunahamasisha ushirikiano kati ya wananchi na wahifadhi katika kulinda mazingira yetu

Mradi wa FOLUR unatekelezwa kwa miaka mitano kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani, ambapo katika Tanzania Bara unatekelezwa katika Halmashauri ya Mlimba kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni sita.