Pambazuko FM Radio

Kilombero yapanda miti 2000 kuadhimisha Muungano

26 April 2026, 14:45

Picha ya Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, watumishi TFS na wanafunzi sekondari ya wasichana Ifakara (Picha na Kuruthumu Mkata)

Katika kumbukizi ya Muungano iliyoambatana na zoezi la upandaji miti Mkuu wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi

Na Katalina Liombechi

Wilya ya Kilombero imeungana na Watanzania wengine kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kupanda miti 2000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuenzi Muungano huo pamoja na kutunza mazingira.

Kati ya miti hiyo, miti 1500 imepandwa katika Halmashauri ya Mlimba, huku miti 500 ikipandwa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, akiwa mgeni rasmi katika kumbukizi hiyo iliyoambatana na zoezi la upandaji miti amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Aidha, ameziagiza taasisi za serikali na binafsi kujenga utamaduni wa kupanda miti kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Picha ya DC Kyobya akizungumza katika zoezi la upangaji miti Ifakara(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya DC Kyobya

Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilayani Kilombero, Mhifadhi Zarina Shaweji, amesema miti ina mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi huki akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchukua miche ya miti inayotolewa bure na wakala hiyo ili kuipanda katika maeneo yao.

Picha ya Mhifadhi Zarina Shaweji Meneja TFS Kilombero(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Meneja wa TFS Kilombero

Naye Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilaya ya Kilombero, Benitho Miwandu, amepokea wito huo na kuahidi kushirikiana katika juhudi za upandaji miti huku Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Selemani Vasomana, apongeza jitihada hizo na kuwataka wanafunzi wa shule hiyo kuitunza miti iliyopandwa kwa uangalifu mkubwa.

Sauti ya Benitho Miwandu Mwenyekiti NGO’s Kilombero

Kwa upande wake, mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara, Miriam, ameahidi kuitunza miti hiyo na kuendelea kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Picha ya DC kyobya akipanda mti na wanafunzi wa shule ya sekondari Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Miriam Ally Mwanafunzi

Maadhimisho ya siku ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar hufanyika kila Ifikapo Aprili 26,ambapo kwa mwaka huu 2026 yanaadhimishwa chini ya kaulimbiu isemayo Muungano: Amani Umoja na Mshikamano ni Msingi wa Maendeleo Endelevu.