Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
28 November 2026, 20:10

Changamoto ya wazazi kutowasiliana na watoto wao na kutowasikiliza wanapojaribu kueleza matatizo yao imetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuwaweka vijana katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Na Katalina Liombechi
Wazazi wametakiwa kuimarisha mawasiliano na watoto wao kwa kuwasikiliza na kuwapa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili, ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.
Hayo yameelezwa katika semina ya siku tatu ambayo imeanza leo Novemba 28, 2026, katika Kanisa Kuu la KKKT Milola, iliyoandaliwa na kanisa hilo kupitia Kituo cha huduma ya Mtoto na Kijana kwa lengo la kuwajengea vijana misingi imara ya kiroho, kujitambua, kujithamini na kujilinda dhidi ya ukatili.
Mratibu wa kituo hicho, Nancy Tangani, amesema hiyo inalenga kuwafikia vijana 200, akibainisha kuwa changamoto zinazowakabili zinaonesha umuhimu wa kuwapatia malezi ya kiroho pamoja na elimu ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa semina hiyo kutoka TASLI, Alexander Mpwaga, amewataka wazazi na jamii kuwapa vijana nafasi ya kusikilizwa, kuwajengea hali ya kujithamini na nguvu ya ndani ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali, hususan zinazohusiana na balehe.

Sauti ya Mpwaga
Baadhi ya vijana walioshiriki semina hiyo wamesema mafunzo hayo yamekuwa msaada kwao kwa kuwa yanawapa uelewa kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Mmoja kati ya wazazi waliohudhuria semina hiyo wamesema wamepata mafunzo ya umuhimu wa kuwasikiliza watoto wao na kuepuka kuwakaripia wanapohitaji kueleza changamoto zinazowakabili.

Semina hiyo ambayo inafanyika katika kipindi cha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia imewalenga vijana wenye umri kati ya miaka 12_18 na yanafanyika kwa ushirikiano kati ya KKKT na TASLI, chini ya ufadhili wa Shirika la Compassion Tanzania.