Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
10 October 2026, 17:06
Wakulima wengi wa Bonde la Kilombero bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani, hali inayochangia baadhi yao kutofahamu manufaa yake katika kuongeza kipato kupitia kilimo cha ushirika, nasi tunaendelea kutoa elimu zaidi ya faida zake-Meneja wa Ifakara AMCOS

picha ya Zao la Mbaazi, Picha kwa Hisani ya Mtandao
Na Henry Mwakifuna
Meneja wa Ifakara AMCOS, Tunu Rajabu Mahupa, amesema wakulima wengi katika Bonde la Kilombero bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani, hali inayochangia baadhi yao kutofahamu manufaa yake katika kuongeza kipato kupitia kilimo cha ushirika.
Akizungumza katika kipindi cha Kilimo na Mifugo kinachorushwa na Pambazuko FM, Mahupa amesema elimu kwa wakulima ni muhimu ili waweze kuelewa namna mfumo huo unavyofanya kazi, kuanzia maandalizi ya mazao hadi uuzaji na upatikanaji wa malipo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ifakara AMCOS, Juma Saidi Ndikanye, amesema baadhi ya wakulima wanaelewa mfumo huo kwa kuzingatia zaidi kupeleka mazao na kulipwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuwaelimisha zaidi kuhusu dhana na manufaa ya stakabadhi ghalani.
Mahupa amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuwasilisha mazao yaliyo safi na yenye ubora unaotakiwa ghalani, akieleza kuwa malipo kwa wauzaji hufanyika ndani ya saa 48 baada ya mnada, kwa mujibu wa utaratibu wa mfumo huo.
Naye mjumbe wa bodi ya Ifakara AMCOS, Said Matengo, amesema stakabadhi ni uthibitisho muhimu katika mfumo huo, hivyo wakulima wanapaswa kuelewa umuhimu wake na namna unavyohusiana na uuzaji wa mazao kupitia vyama vya ushirika.
Ifakara AMCOS, yenye wanachama 60, inakusanya mazao ya mbaazi na ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Mfumo huo unalenga kuwawezesha wakulima kushiriki katika masoko ya mazao kwa utaratibu wa ushirika na kuongeza fursa za kuboresha kipato chao.
saauti ya Viongozi wa Bodi ya Ifakara AMCOS