Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 September 2026, 19:18

“Halmashauri ya Mji wa Ifakara imesema haitamvumilia mtu au kikundi kitakachoshindwa kurejesha fedha hizo bila sababu za msingi”Kassim Faya Nakapala -Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara .
Na El;ias Maganga
Halmashauri ya Mji wa Ifakara imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 789.2 kwa vikundi 84 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2025/2026. Fedha hizo zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo iliyofanyika katika viwanja vya Soko Kuu la Ifakara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Pilly Kitwana, amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Kassim Nakapala, amevitaka vikundi vilivyonufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika. Amesisitiza kuwa halmashauri haitamvumilia mtu au kikundi kitakachoshindwa kurejesha fedha hizo bila sababu za msingi.
Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Kassim Nakapala
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa shughuli zilizokusudiwa na kuepuka matumizi yasiyo na tija. Pia amewaagiza maafisa maendeleo wa kata kufuatilia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa mikopo hiyo na kuendelea kutoa elimu kwa vikundi ambavyo bado havijasajiliwa ili vipate fursa ya kunufaika.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa kuwawezesha kupata mtaji unaowasaidia kuboresha maisha yao.
Wamesema watahakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kuendelea kujenga uaminifu na kuwezesha vikundi vingine kupata fursa hiyo.

Picha ya Baadhi ya wanufaika wa mikopo.(Picha na Elias Maganga)
Sauti ya Baadhi ya wanufaika wa mikopo.