Pambazuko FM Radio

Uhifadhi Wasaidia Ujenzi wa Zahanati ya Mpofu-Mlimba

20 November 2026, 21:04

Picha ya baadhi ya viongozi na wananchi katika eneo la ujenzi wa Zahanati ya Mpofu(Picha na Katalina Liombechi)

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa uhifadhi na kufadhiliwa na Hempel Foundation pamoja na Aage V. Jensen Charity Foundation

Na Katalina Liombechi

Wananchi wa Kijiji cha Mpofu, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, wanatarajia kunufaika na shilingi milioni 10 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho, kupitia Mkataba wa Uhifadhi uliosainiwa kati ya kijiji hicho na Shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP), kwa kushirikiana na Hifadhi ya Mazingira Asili ya Kilombero.

Mkataba huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Mandhari ya Milima ya Udzungwa (Udzungwa Landscape Strategy – ULS), unaolenga kuimarisha uhifadhi wa misitu na wanyamapori huku jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zikinufaika na miradi ya maendeleo.

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa uhifadhi na kufadhiliwa na Hempel Foundation pamoja na Aage V. Jensen Charity Foundation.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayo katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Novemba 19,2026 Kijijini hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la STEP Frank Lihwa ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuifanya jamii kuwa sehemu muhimu ya juhudi za uhifadhi kwa kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na kulinda rasilimali za asili.

Picha ya Frank Lihwa Mkurugenzi STEP(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Frank Lihwa Mkurugenzi STEP 1

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba  Salmin Misango amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia masharti ya mkataba huo, ambao unawataka kushiriki katika kuzuia ukataji miti na uwindaji haramu, kudhibiti moto wa misitu, kulinda vyanzo vya maji na bioanuwai, pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Picha ya Salmin Misango Mwanasheria Halmashauri ya Mlimba(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Salmin Misango Mwanasheria Mlimba

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mpofu wameeleza kufurahishwa na makubaliano hayo, wakisema msaada wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati utachangia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuongeza hamasa ya jamii kushiriki katika shughuli za uhifadhi.

Picha ya baadhi ya wananchi wakiwa katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uhifadhi(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za wananchi

Mradi wa Mandhari ya Milima ya Udzungwa (Udzungwa Landscape Strategy – ULS), ni mkakati wa miaka 20 huku kwa mujibu wa Frank Lihwa waanaamini mhimili mkubwa wa kufanikisha uhifadhi ni wananchi wenyewe ndio maana wanajikita kuinua hali zao na kuchangia maendeleo.

Sauti ya Frank Lihwa Mkurugenzi STEP 2

Mkataba huo utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, huku STEP, Hifadhi ya Mazingira Asili ya Kilombero na viongozi wa kijiji wakifanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wake na kwamba ushirikiano huo unaonesha namna uhifadhi unavyoweza kuwa chachu ya maendeleo kwa kuunganisha ulinzi wa mazingira na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.