Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
20 September 2026, 15:48

Uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele unadhibitiwa kupitia sheria na kanuni za mazingira. na pia matumizi ya eneo yanapaswa kuendana na shughuli iliyoruhusiwa katika eneo hilo, muhimu matumizi ya vizuia kelele ni muhimu katika maeneo kama baa, kumbi za burudani na hata baadhi ya maeneo ya ibada, ili kupunguza sauti na mitetemo inayoweza kuwafikia watu walioko nje ya eneo husika-Salome Mayenga-Afisa Mazingira Ifakara Mji
Na Henry Mwakifuna
Kelele zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, lakini zinapozidi kiwango kinachokubalika, huwa kero kwa wananchi, hasa nyakati za usiku. Muziki unaopigwa kwa sauti kubwa katika maeneo ya biashara na maeneo ya makazi ni miongoni mwa vyanzo vinavyolalamikiwa zaidi.
Kwa upande wa wamiliki wa baa, baadhi yao wanasema hupiga muziki kwa sauti kubwa ili kuvutia wateja. Hata hivyo, wanapaswa kuzingatia majirani na muda unaoruhusiwa, kwa kuwa kupunguza sauti kunaweza kuathiri biashara zao. Hivyo, ni muhimu biashara kuendeshwa kwa kuzingatia mazingira yanayowazunguka.
Wenyeviti wa mitaa wameeleza kuwa uchafuzi wa kelele ni changamoto inayojitokeza katika baadhi ya maeneo, hususan kwenye baa na vilabu vya kienyeji. Wamekuwa wakitoa elimu na maonyo kwa wanaokiuka, na pale tatizo linapoendelea, hatua za kisheria ikiwemo faini huchukuliwa. Pia, wameeleza umuhimu wa muziki kupigwa ndani ya maeneo ya biashara na wahusika kuwa na vibali vinavyohitajika.
Afisa Mazingira Salome Mayenga wa Halmashauri ya Ifakara Mji anasema uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele unadhibitiwa kupitia sheria na kanuni za mazingira. Anaeleza kuwa matumizi ya eneo yanapaswa kuendana na shughuli iliyoruhusiwa katika eneo hilo, huku wahusika wakitakiwa kuzingatia taratibu na kupata vibali kutoka mamlaka husika, ikiwemo pale inapohitajika kibali cha shughuli za burudani na utamaduni.
Aidha, matumizi ya vizuia kelele ni muhimu katika maeneo kama baa, kumbi za burudani na hata baadhi ya maeneo ya ibada, ili kupunguza sauti na mitetemo inayoweza kuwafikia watu walioko nje ya eneo husika. Kwa kufanya hivyo, jamii inaweza kupunguza kero za kelele na kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinafanyika bila kuathiri haki ya wengine ya kuishi katika mazingira tulivu.
Sikiliza Kona ya Jamii juu ya Athari za Uchafuzi wa Mazingira kwa Sauti