Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
29 September 2026, 12:13
“Kukubali mawazo ya wataalamu kuhusu masuala ya mipaka ni jambo la msingi. Viongozi, wakiwemo wanasiasa, wanapaswa kukubaliana na ushauri wa wataalamu, bila kujali kama wanapendezwa au hawapendezwi na ushauri huo. Cha muhimu ni kufuata sheria.”–Andrew Matajiri-Makamu Mwenyekiti Ifakara Mji

Andrew Matajiri, Makamu Mwenyekiti wa Halamashauri ya Ifakara Mji akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika Uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi picha na Jack Line
Na Henry Mwakifuna
Viongozi wametakiwa kuzingatia ushauri wa wataalamu katika kutatua migogoro ya mipaka na masuala ya ardhi, badala ya kutumia nafasi zao za uongozi kuingilia utekelezaji wa sheria.
Wito huo umetolewa na Mheshimiwa Andew Matajiri, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wakati akizungumza baada ya kupewa nafasi katika uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi uliofanyika katika eneo la Kata ya Kidatu, Wilaya ya Kilombero.
Matajiri amesema baadhi ya migogoro inaweza kuchangiwa na viongozi wenyewe pale wanaposhindwa kuzingatia ushauri wa wataalamu katika masuala yanayohitaji utaalamu, hususan katika utatuzi wa migogoro ya mipaka.
Amesema viongozi, wakiwemo wanasiasa, wanapaswa kuwa tayari kukubali ushauri wa wataalamu hata pale ambapo ushauri huo hauendani na matarajio au matakwa yao, kwa kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha maamuzi yanafanyika kwa kuzingatia sheria.
sauti ya Makamu Mwenyekiti wa Ifakara Mji
Upande mwingine Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Rashid Semgoya amesisitiza kuwa Migogoro baina ya Vijiji au kata na kata ni ya kipekee na suluhisho linaletwa na Wataalam ambao wanahitaji Ushirikiano baina ya Viongozi.
Sauti kaimu Mkurugenzi wa Mji Ifakara

Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika kupata huduma ya kliniki ya Ardhi kata ya Kidatu Wilayani Kilombero picha na Henry Mwakifuna
Baadhi ya Wananchi wanaofika katika Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika Kata ya Kidatu, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wameeleza umuhimu wa huduma hiyo katika kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusiana na ardhi.
Sharifa Msuya, mkazi wa Mkamba, Kijiji cha Kidatu, ambaye amefika katika kliniki hiyo kufuatilia upatikanaji wa hati mpya ya kiwanja, amewataka wananchi wenzake kutumia fursa hiyo kupata huduma za ardhi kutoka kwa wataalamu.
Sharifa amesema wananchi wanapaswa kutumia muda ambao wataalamu wapo katika eneo hilo kufuatilia masuala yao ya ardhi na kupata ufafanuzi wa changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Peter Mushi, mkazi wa Mkamba B, amesema baadhi ya changamoto za maeneo zinahitaji ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato wa upimaji na uwekaji wa mipaka.
Mushi amesema kwa uzoefu wake, baadhi ya maeneo yalianza kugawiwa tangu miaka ya 1980 bila ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi, hali ambayo amesema bada ya kuanza Upimaji imeendelea kuleta changamoto katika masuala ya mipaka.
sauti ya baadhi ya Wananchi
Kliniki hiyo ya Ardhi ilianza Septemba 28 na inatarajiwa kutoa huduma hadi Oktoba 2 mwaka huu.