Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
19 October 2026, 22:28

Ushiriki wa kampuni ya Agricom Limited Africa katika tamasha la Kilombero International Bantu Festival umetajwa kuwa fursa muhimu kwa wakulima wa halmashauri ya mji wa Ifakara kupata zana bora za kisasa kuelekea msimu mpya wa kilimo, ili kuongeza tija, uzalishaji, na kuinua uchumi wa kaya zao.
Na: Isidory Mtunda
Ushiriki wa kampuni ya zana za kilimo ya Agricom Limited Africa katika Tamasha la Kilombero International Bantu Festival, umetajwa kuwa chachu kubwa ya kuboresha sekta ya kilimo na kuinua uchumi wa wananchi na wakulima waliotembelea tamasha hilo.

Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Tamasha hilo, Godlove Nyagawa, alipozungumza na Pambazuko FM Radio kuhusu mchango wa wadau mbalimbali walioshiriki katika maonyesho hayo kutoa elimu na fursa za kiuchumi.
Naye Meneja wa Agricom Limited Africa Tawi la Ifakara, Graceana Makungu, amewakaribisha wakulima kufika katika banda lao kujipatia zana za kisasa zitakazowasaidia kurahisisha shughuli za kilimo na kuongeza tija kuelekea msimu mpya wa kilimo.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima walioshiriki tamasha hilo, William Kawawa na Hashim Mtambo, wameeleza kuwa matumizi ya zana bora yanakwenda kuwakomboa kutoka kwenye kilimo cha jembe la mkono na kuwawezesha kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari mbili hadi ekari kumi.
Tamasha la Kilombero International Bantu Festival lilifanyika katika uwanja wa CCM Tangani (uwanja wa taifa) uliopo halmashauri ya mji wa Ifakara kuanzia Oktoba 16, 2026, likijumuisha taasisi na wadau mbalimbali wakiwemo RUWASA, EFTA, NSSF, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis, TARI, TFS na wengine wengi.