Nuru FM

Chelsea yaruhusiwa kuuza tiketi

25 March 2022, 7:02 am

CHELSEA itaruhusiwa kuuza tiketi za michezo ya ugenini, mechi za mataji zinazohusisha timu ya wanawake baada ya serikali ya Uingereza kufanya mabadiliko kwenye leseni maalum ya klabu hiyo.

Klabu hiyo haikuweza kuuza tiketi tangu mmiliki Roman Abramovich alipowekewa vikwazo na serikali kama sehemu ya majibu yake kwa uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.

Chini ya leseni iliyobadilishwa, mapato yatokanayo na mauzo ya tiketi yataenda moja kwa moja kwenye Ligi Kuu.

22472776

Hatua hiyo ina maana kwamba Chelsea wataweza kuuza tiketi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid Aprili 6 na nusu fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Wembley Aprili 16 dhidi ya Crystal Palace.

Mashabiki wa ugenini wanaweza kununua tiketi za michezo ya Ligi Kuu pale Stamford Bridge, na mapato yataenda kwa Ligi Kuu.

Chelsea wameomba kwamba fedha zozote zinazotokana na mauzo ya tiketi, ambazo klabu ingekuwa nazo kwa kawaida, zitolewe kwa waadhiriwa wa vita nchini Ukraine.

Waziri wa Michezo, Nigel Huddleston alisema: “Ningependa kuwashukuru mashabiki kwa uvumilivu wao wakati tumeshirikiana na mamlaka ya soka ili kufanikisha hili.

“Tangu Roman Abramovich alipoongezwa kwenye orodha ya vikwazo vya Uingereza kwa uhusiano wake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin tumefanya kazi kubwa kuhakikisha klabu inaweza kuendelea kucheza soka huku tukihakikisha sheria ya vikwazo inaendelea kutekelezwa.”