Mpanda FM
Mpanda FM
8 September 2025, 2:49 pm

“wako tayari kufanya kazi ya kilimo na ufugaji ili waweze kujiinua kiuchumi “
Na Anna Milanzi-Katavi
Vijana manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wameshauriwa kuhakikisha wanakuwa na maarifa ili waweze kutunza fedha na kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamejiri katika muendelezo wa mijadala ya vijana inayoandaliwa na mwandishi wa habari wa Mpanda Redio FM Anna Milanzi,ambapo vijana hao wameonesha kuhitaji Fedha zaidi kuliko kupata kwanza maarifa ya kuzitunza na nyenzo ya kuzalisha fedha.
Afisa maendeleo kutoka katika taasisi ya tuelimike Bavuga Sadock na mdau wa masuala ya kilimo na biashara ambae pia ni afisa kilimo John Kapesula wamezungumza na vijana hao na kuwaeleza umuhimu wa kuthamini fedha unayoipata kwa kufanya shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ili kuindeleza fedha uliyonayo.

Kupitia elimu hiyo waliyoipata imebadilisha mtazamo kwa vijana hao huku wengi wao wakieleza kuwa wako tayari kufanya kazi ya kilimo na ufugaji ili waweze kujiinua kiuchumi kazi ambayo hapo awali hawakuona umuhimu wa kuifanya.
Kwa mujibu wa utafiti wa kilimo wa mwaka 2022/2023 uliofanywa na ofisi ya takwimu( NBS) na ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali (OCGS) kwa kushirikiana na wizara zinazoongoza sekta ya kilimo imeonesha kuwa sekta ya kilimo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi nchini,upatikanaji wa ajira,na kupunguza umasikini huku kilimo kikichangia asilimia 26.5 ya pato la taifa.