

27 March 2025, 4:51 pm
Picha ya meneja wa mradi wa VUMA Henry Bendera. Picha na Restuta Nyondo
“Tumebaini vijana wengi hukimbilia kwa waganga kupata matibabu”
Na Restuta Nyondo
Zaidi ya waganga wa tiba asili 80 kutoka katika wilaya za Mpanda na Tanganyika mkoani Katavi wamepatiwa mafunzo juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, utoaji huduma salama na lishe .
Mafunzo hayo ya siku 3 yamefanyika katika ukumbi wa Katavi Resort yaliyoandaliwa na shirika la Plan International Tanzania kupitia mradi wa vijana na ubora, malengo na afya (VUMA) unaolenga kuiboresha afya ya uzazi kwa vijana na kuwawezesha kiuchumi.
Wakizungumza na Mpanda Radio FM baadhi ya waganga wa tiba asili wamesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia katika utoaji wa huduma kwa jamii wanazohudumia hususani kuchukua hatua pale wanaposhindwa kwa kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma.
Henry Bendera ni meneja Mradi wa VUMA mkoani Katavi amesema kuwa wamefanya mafunzo kwa wataalamu hao kutokana na tafiti zimebaini kuwa vijana wengi hukimbilia kwa waganga kupata matibabu na msaada hususani changamoto za afya ya uzazi.
Mafunzo hayo yanatarajia kuwafikia wataalamu wa tiba asili 116 na viongozi wa kimila 50 kutoka katika wilaya ya Tanganyika, Mpanda na Mlele.