Jamii FM

Wananchi walia na uchakavu wa madarasa shule ya msingi Litembe

14 November 2024, 18:07 pm

Mwonekano wa nje wa madarasa ya shule ya Msingi Litembe na hili ni darasa la tano(Picha na Musa Mtepa)

Shule ya Msingi Litembe inapatikana katika kata ya Madimba halmsahauri ya Mtwara Vijijini mkoani Mtwara ambapo hadi kufikia Novemba 14, 2024 ina jumla ya wanafunzi 267 wanaosoma katika shule hiyo.

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Kijiji cha Litembe, Kata ya Madimba, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wameelezea wasi wasi mkubwa kuhusu usalama wa watoto wao wanaosoma katika Shule ya Msingi Litembe kutokana na uchakavu na ubovu wa miundombinu ya shule hiyo.

Wakizungumza na Redio Jamii FM leo, Novemba 14, 2024,  wamesema kuwa hali ya madarasa ilivyo imekuwa hatari kwa watoto, na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea taharuki yoyote kwa watoto hao kutokana na hali mbaya ya miundombinu.

Wananchi hao wameiomba serikali kuu kuangalia kwa jicho la tatu hali ya shule hiyo, na kutoa msaada wa haraka kwa kufanya marekebisho ya madarasa au hata kujenga majengo mapya ili kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira salama

Sauti ya 1 wananchi wa Kijiji cha Litembe

Wakazi wa Kijiji cha Litembe, wakiwemo Zuhura Mohamed na Ashura Mkwakwati, ambao wanaishi karibu na shule hiyo, wamesema kuwa kutokana na ubovu wa madarasa, walimu hulazimika kuwaruhusu  watoto kurudi nyumbani katika kipindi cha Masika na  Wakati mwingine, wanafunzi hutumia nyumba za jirani kuhifadhi daftari zao ili kuepuka na kuathiriwa na mvua.

Sauti ya Zuhura Mohamed na Ashura Mkwakwata Wakazi wa Kijiji cha Litembe

Diwani wa Kata ya Madimba, Issa Kujebweja, amesema kuwa kama mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata, changamoto kubwa inayomkabili ni hali mbaya ya miundombinu ya shule hiyo huku  akiiomba halmashauri na serikali kuu kuchukua hatua za haraka ili kulinda usalama wa watoto wanaosoma katika shule hiyo.

Sauti ya Issa Kujebweja Diwani wa kata ya Madimba

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abeid Abeid Kafunda, amekiri kuwa shule ya Msingi Litembe inakabiliwa na hali mbaya ya miundombinu na kwamba halmashauri inafanya mipango ya ukarabati .

Kafunda amesema kuwa, pindi fedha za ukarabati wa shule kongwe zitakapopatikana,atawasilisha katika  baraza la halmashauri ili kuona jinsi ya kusaidia shule hiyo na kuboresha miundombinu yake.

Sauti ya 1 Abeid Abeid Kafunda mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Mtwara vijijini

Hata hivyo, Kafunda ameelezea changamoto nyingine, akisema kuwa shule hiyo haikufikia vigezo vya kupata mradi wa “BOOST” kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi.

Amesema licha ya changamoto hiyo, halmashauri inaendelea kutafuta njia nyingine za kusaidia shule hiyo na kuboresha hali ya miundombinu.

Sauti ya 2 Abeid Abeid Kafunda mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mtwara Vijijini.