Diwani Madimba aitaka halmashauri kuiangalia jicho la tatu shule ya msingi Litembe
8 November 2024, 09:40 am
Miundombinu ya shule ya Msingi Litembe hali yake Mbaya hivyo halmashauri isipochukua hatua kuelekea msimu wa mvua kunauwezekano wa kufungwa kutokana na majengo yake kuchakaa.
Na Musa Mtepa
Diwani wa kata ya Madimba, Idrisa Ali Kujebweja, ameitaka Halmashauri ya Mtwara Vijijini kuchukua hatua za haraka kuhusu hali ya uchakavu wa shule ya Msingi Litembe iliyoko katika kata hiyo.
Akizungumza katika kikao cha robo ya kwanza kilichofanyika Novemba 7, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Mustafa Sabodo, Diwani Kujebweja amesema kuwa kutokana na hali mbaya ya miundombinu ya madarasa katika shule hiyo, ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, kuna hatari ya shule hiyo kufungwa.
Ameongeza kuwa, endapo hali hiyo itaendelea, watoto watashindwa kupata elimu na badala yake kuwa watoto wa mitaani.
Baadhi ya madiwani wakiongozwa na Diwani wa kata ya Ndumbwe, Abduly Mahupa, wamekubaliana na wito huo na kuhimiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kurekebisha hali hiyo na kuhakikisha shule hiyo inakuwa katika mazingira bora yatakayowashawishi wanafunzi na walimu kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abeid Kafunda, amekiri kuwepo kwa changamoto ya uchakavu wa shule hiyo.
Amesema kuwa tayari wameanza kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuleta mradi wa “Boost”, ingawa mradi huo umekuwa ukilenga shule zenye wanafunzi wengi. Kafunda ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi katika madarasa.
Aidha, Kafunda ameongeza kuwa Halmashauri inafikiria kutumia fedha zitakazopatikana kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe ili ziweze kutumika kwa ukarabati wa shule ya Msingi Litembe.
Kikao hicho cha robo ya kwanza kilikutanisha madiwani kutoka kata zote za halmashauri hiyo, ambapo kila diwani alijadili maendeleo ya kata yake na kutoa mapendekezo ya hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuboresha huduma katika maeneo yao.