Wanahabari Mtwara wahimizwa kuwasemea watoto wenye mahitaji maalum
7 November 2024, 11:56 am
Walimu wenye ujuzi wa kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni wachache na wakati mwingine hata Mwalimu mkuu wa baadhi ya shule hawafahau na hawana uelewa juu ya mkakati na mwongozo wa Elimu jumuishi
Na Musa Mtepa
Waandishi wa Habari mkoani Mtwara wamehimizwa kuchangia kwa nguvu katika kuhamasisha serikali kuajiri walimu wenye ujuzi wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu, ili waweze kupata elimu sawa na wenzao.
Wito huo umetolewa na Afisa Mradi wa Sauti Zetu, Ndugu Deogratius Makoti, wakati akizungumza na waandishi wa habari tarehe 6 Novemba 2024, baada ya mafunzo mafupi kwa wanahabari.
Makoti amesema kuwa watoto wenye mahitaji maalumu mara nyingi wamekuwa wakisahaulika, hali inayopelekea kushindwa kupata haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na haki ya elimu.
Anasisitiza kuwa waandishi wa habari wanalo jukumu kubwa katika kuhakikisha jamii na serikali wanaelewa umuhimu wa kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu bora na yenye usawa kama watoto wengine.
Aidha, Makoti amesema kuwa utafiti mdogo uliofanywa na MTWANGONET umeonyesha kuwa changamoto kubwa zinazowakumba watoto wenye mahitaji maalumu zinachangiwa na serikali kutotekeleza kikamilifu mwongozo wa Elimu Jumuishi, ambao unatoa maelekezo ya namna ya kuwasaidia watoto hao, ikiwemo kuajiri walimu wenye ujuzi wa kuwafundisha na kuwatambua wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wao, waandishi wa habari mkoani Mtwara, Sospeter Magumba na Sijawa Omari, wamesema kuwa jukumu lao ni kutoa taarifa, kufanya ushawishi na utetezi kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu watoto wenye mahitaji maalumu.