

2 February 2025, 12:02 pm
Kijiji cha Makome B kipo umbali wa zaidi ya Kilomita 35 kutoka makao makuu ya mkoa wa Mtwara na kipo katika kata ya Mbawala,Halmashauri ya Mtwara vijijini kilichozungukwa na Milima na Mabonde pamoja na misitu asili
Na Musa Mtepa
Kutokana na changamoto ya umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 15, wazazi na wananchi wa Kijiji cha Makome B, kata ya Mbawala, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wameamua kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu kwa urahisi na kuondoa adha wanayopata kwa kutembea umbali mrefu kila siku.
Wananchi hao wakizungumza na Jamii FM Radio na wameelezea jinsi umbali huo unavyowafanya watoto wao kuamka saa kumi alfajiri ili kujiandaa na kwenda shule ya sekondari Umoja iliyopo katika Kijiji cha Mdui.
Fatuma Abdala Fundi, mzazi mwenye mtoto anayeenda shule ya Umoja, amesema kuwa umbali huo unahatarisha mustakabali wa watoto wao, kwani wengi wao wanashindwa kumaliza elimu ya sekondari kutokana na uchovu na changamoto za usalama.
Wananchi wengine, Hassani Chihako na Ahmadi Mnyamba, wameongeza kuwa umbali mrefu unakwamisha wasichana kumaliza elimu ya sekondari kwa usalama, na kuna hatari ya kukutana na vishawishi vinavyoweza kuathiri masomo yao, ikiwemo kupata ujauzito na kuacha shule.
Kutokana na changamoto hiyo, wananchi wa Kijiji cha Makome B wameanzisha ujenzi wa shule ya sekondari kwa kujenga boma lenye vyumba vitatu na ofisi moja ya walimu, ambayo tayari imefikia hatua ya kufunga linta. Hata hivyo, wanahitaji msaada zaidi kutoka kwa serikali na wadau ili kukamilisha ujenzi huo na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Makome B, Bakari Mkanjalanga, amekiri kuwepo kwa changamoto ya umbali mrefu na kuelezea juhudi zinazofanywa na wananchi kujenga shule hiyo kwa kuchangia shilingi 12,000 kwa kila mwananchi.
Hata hivyo, ameeleza kuwa hapo awali walikubaliana na Wananchi kukatwa kiasi kidogo cha fedha kupitia zao la korosho ili kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ila hali imekuwa tofuati na matarajio , kwani hadi kufikia Januari 30, 2025, fedha za wananchi hazijapatikana kutoka kwa chama cha ushirika cha Umoja, kutokana na kutokana na mkanganyiko na utata wa taarifa za fedha.
Wananchi wa Kijiji cha Makome B wanaendelea kuomba msaada na ushirikiano kutoka kwa serikali na wadau wengine ili kuhakikisha ujenzi wa shule unakamilika na kutoa fursa kwa watoto wa kijiji hicho kupata elimu kwa usalama zaidi.