Mpanda FM
Mpanda FM
16 February 2026, 8:30 pm

“Mradi ni fursa muhimu katika juhudi za kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga“
Na Ben Gadau -Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, amezindua mradi wa THAMINI UHAI unaolenga kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga mkoani Katavi.
Mhe. Mrindoko amewataka viongozi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yake.
Amesema mradi ni fursa muhimu katika juhudi za kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza na kutumia kikamilifu huduma zinazotolewa kupitia mradi kwa manufaa ya afya ya mama na mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Thamini Uhai, Banzi Msumi, amesema kuwa tangu mwaka 2019 mradi huo, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na TAMISEMI, umejikita katika ujenzi na ukarabati wa wodi za wazazi, vyumba vya watoto njiti, pamoja na utekelezaji wa mpango wa msindikizaji wa mjamzito katika vituo nane vya afya vilivyopo katika halmashauri zote tano za Mkoa wa Katavi.
Mradi wa THAMINI UHAI unatekelezwa kwa ufadhili wa Bloomberg Philanthropies na Gates Foundation. Ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa kuanzia Septemba 2025 hadi Juni 2030 katika mikoa ya Geita, Katavi na Kigoma. Mradi unalenga kuimarisha huduma za kliniki ya wajawazito, huduma za dharura za mama na mtoto, pamoja na kuboresha huduma za watoto wachanga ili kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma salama na zenye staha.