Mpanda FM
Mpanda FM
30 July 2025, 7:08 pm

Mkuu wa mkoa wa Katavi akitoa maelekezo kwa watumishi wa umma. Picha na Anna Mhina
“Ninyi ni watumishi wa umma mnapaswa kutoa huduma bora kwa wananchi”
Na Anna Mhina
Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko amewataka maafisa tarafa na watendaji kata kuwa waadilifu kwa kuzingatia kanuni na sheria za utumishi katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao.
Mrindoko ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye kufunga mafunzo ya maafisa tarafa na watendaji kata ambao ni waajiriwa wapya kutoka mkoa wa Rukwa, Kigoma na Katavi na kuwasisitizia wajibu wao mahala pa kazi.
Hamisi Mkunga ni mkurugenzi msaidizi usimamizi wa rasilimali watu kutoka ofisi ya Rais (TAMISEMI) ameeleza lengo la mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzie Sola Balana ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuandaa mafunzo yaliyowapa uwezo na kuahidi kwenda kuyatendea kazi.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji kata yamefanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Katavi na kuhudhuriwa na watendaji kata 70 na maafisa tarafa 9 kutoka katika mikoa hiyo mitatu.