

27 March 2025, 4:33 pm
Picha ya Katibu wa CHADEMA wilaya ya Mpanda Richard Mponeja. Picha na Edda Enock
“Msimamo wetu ni kuhakikisha kuwa na uchaguzi huru, wa haki na usalama”
Na Edda Enock
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Kimetoa tamko kwa kauli ya Katibu Itikadi na Uenezi Na Mafunzo CCM Taifa Amos Makalla ya CHADEMA kununua virusi vya Ebola na Mpox kwa lengo la kuzuia na kuhatarisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Baadhi ya wanachama wa Chama hicho Wakizungumza na mpanda Radio Fm wamesema kuwa kauli hiyo ya kiongozi wa CCM ni uchochezi na jaribio la kupotosha umma na kuharibu sifa ya chama hicho.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA wilaya ya Mpanda Richard Mponeja amesema kuwa msimamo wao ni kuhakikisha kuwa na uchaguzi huru, wa haki na usalama, na watahakikisha haki ya kupiga kura inaheshimiwa kwa kila Mtanzania.
Ikumbukwe kiongozi huyo wa chama tawala nchini alinukuliwa akitoa kauli hiyo Machi 22 mwaka huu wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM, Mkoa wa Simiyu.
Uchaguzi mkuu wa kuchagua viongozi mbalimbali unatarajiwa kufanyika Octoba 2025 nchini Tanzania.