

4 March 2025, 2:24 pm
Picha ya baraza la machinga wilaya ya Mpanda. Picha na Samwel Mbugi
“Tumeazimia kuwainua machinga kwa kuwakopesha mikopo yenye riba nafuu”
Na Samwel Mbugi
Baraza la machinga wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wameazimia kuwainua wafanyabiashara wadogo kwa kushirikiana na taasisi za kifedha kwa kuwakopesha mikopo yenye riba nafuu.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa shirikisho la machinga wilaya ya Mpanda Khaji Said Mponda kwenye mkutano mkuu wa baraza la machinga uliofanyika ukumbi wa mikutano Mpanda hotel ambapo baraza hilo limeenda sambamba na kukabidhi vyeti kwa wadau mbalimbali waliofanya vizuri kwa kushirikiana na shirikisho hilo.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi ambaye ni mstahiki meya wa manispaa ya Mpanda katibu wa shirikisho la machinga wilaya ya Mpanda Peter Kosmas Mwansile amesema shirikisho limejiwekea malengo ya kujenga misingi ya upendo na kuinuana kiuchumi.
Mwenyekiti wa shirikisho la machinga mkoa wa Katavi Michael Ernest amesema kuwa wafanyabiashara wadogo wamepata upendeleo kwa uongozi wa awamu ya sita kwa kutambuliwa, kupangwa na kupewa vitambulisho vya kuwatambua na kuwawezesha kupata mikopo.
Haidary Sumry Meya wa manispaa ya Mpanda ambae alikuwa mgeni rasmi wa mkutano huo amewatia moyo wafanyabiashara wadogo kuendelea kupambana na wasiogope kukopa kwani nae aliwahi kuwa machinga na kwa sasa ni mfanyabiashara mkubwa kupitia mikopo
Hata hiyo Sumry ameahidi kushirikiana kwa kila jambo na wafanyabiashara wadogo ili kuhakikisha changamoto zote zinazowakumba zinatauliwa kwa wakati