

27 January 2025, 5:30 pm
Picha ya Stuart Kiondo akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Lilian Vicent
“Stendi kuu ya Mizengo Pinda kuna mapungufu katika ukusanyaji wa mapato”.
Na Lilian Vicent
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Katavi imefanikiwa kuokoa fedha kiasi cha shilingi milioni mia moja ishirini na laki tatu (120,300,000) ambazo zilikuwa zitumike vibaya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa robo ya pili iliyoanza oktoba hadi disemba 2024.
Hayo yamesemwa na Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Stuart Kiondo wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo amesema shilingi milioni tisini na moja zimeokolewa za chama cha msingi ILANGU –AMCOS wilaya ya Tanganyika.
Aidha amebainisha kuwa taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi ishirini na saba 27 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.6 katika sekta za elimu ,afya ,ulinzi na usalama na maendeleo ya jamii.
Katika hatua nyingine ameongeza kuwa katika uchambuzi wa mifumo kwenye halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wamebaini katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya stendi kuu ya mizengo Pinda kuna mapungufu yanayopelekea kupoteza fedha nyingi.
Sanjari na hayo Kiondo amesema mikakati kwa kipindi cha Januari hadi Marchi imejipanga kuzuia rushwa, kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2025 na kufanya uchunguzi.