Mmoja afa kwa dalili za kipindupindu
21 January 2025, 6:19 pm
Wananchi wakiwa kwenye mazishi. Picha na Samwel Mbugi
“Wananchi wametakiwa kuzingatia suala la usafi ili kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu”
Na Lilian Vicent
Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Redfusi Gabriel mkazi wa mtaa wa Kasimba kata ya Ilembo manispaa ya Mpanda mkoani Katavi amefariki dunia baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa wa Kipindupindu.
Hayo yamesemwa wakati Mpanda radio fm ikizungumza na wajumbe wa mtaa huo ambapo wamesema kuwa marehemu alipatwa na dalili za kutapika na kuharisha kabla ya kifo chake.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Kasimba Benard Nsima amesema kuwa kila mwananchi ahakikishe anatumia choo bora na kufanya usafi wa mazingira ili kuepuka faini zitakazoanza kutolewa na mamlaka husika ili kuepukana na ugonjwa huo.
Hata hivyo afisa afya kata ya Ilembo Grace Kunchela amesema kuwa dalili zilizopelekea kifo cha marehemu zinaonyesha kuwa ni za kipindupindi, hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kufanya usafi wa mazingira na kutumia choo bora.