Watu wenye ulemavu Katavi walia na TASAF
7 January 2025, 6:34 pm
“Kata ya Mpanda Hotel hakuna mtu mwenye ulemavu ambae amenufaika na TASAF “
Na Samwel Mbugi-Katavi
Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu mkoa wa Katavi Godfrey Albeto Sadala amesema watu wenye ulemavu wanabaguliwa kuingizwa kwenye mradi wa wanufaika wa TASAF.
Hayo yamesemwa katika kikao kilichofanyika kata ya Mpanda hotel ikijumuisha watu wenye ulemavu na viongozi wa kata kikilenga kubaini changamoto zinazowakabili na kuzifanyia ufumbuzi.
Godfrey Albeto Sadala amesema kuwa kata ya Mpanda Hotel hakuna mtu mwenye ulemavu ambae amenufaika na TASAF ambapo amemuomba diwani wa kata kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa yote kuwaingiza watu wenye ulemavu kunufaika na TASAF.
Sauti ya Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu mkoa wa Katavi Godfrey Albeto Sadala
Kwa upande wake Ibrahimu Mzanda mwenyekiti wa Mpanda Hotel akiwawakilisha wenyeviti wa mitaa ya Msasani na Tambukareli amesema kuwa kupitia sera ya utawala bora wamejipanga kutambua makundi ya watu wenye ulemavu kwani wamekuwa wakisahaulika katika jamii.
Sauti ya Ibrahimu Mzanda mwenyekiti wa Mpanda Hotel
Hata hivyo diwani wa kata ya mpanda hotel Hamisi Misigalo amesema kuwa kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa yote watahakikisha walemavu wenye sifa ya kunufaika na mradi wa TASAF wananufaika.
Sauti ya diwani wa kata ya Mpanda Hotel Hamisi Misigalo
Ikumbukwe kuwa lengo la TASAF ni kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa na kulinda maslahi ya watoto wao na jitihada zinaendelea kuwapata viongozi wa TASAF kutolea maelekezo kuhusiana na mgawanyo wa unufaika wa wa mfuko huo kata ya Mpanda Hotel.