Wamiliki wa viwanda vya kubangua karanga Mpanda hotel watakiwa kuhama
24 June 2024, 7:02 pm
Takataka zilizotokana na kazi ya ubanguaji karanga katika eneo la mpanda hotel na kuleta kero kwa wakazi wa maeneo hayo.Picha na Samwel Mbugi
“Mashine zilizopo maeneo hayo zinazalisha taka nyingi ambazo zinasababisha uchafuzi wa mazingira na kupelekea manispaa kuwa chafu“
Na Samweli Mbugi – Katavi
Kufuatia malalamiko ya wananchi wa kata ya Mpanda Hotel mkoa wa Katavi juu ya kero ya viwanda vya kubangulia karanga kusababisha uchafu katika makazi yao pamoja na ugonjwa wa mafua, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph ametoa maagizo kwa wamiliki kuhama eneo hilo na kuzoa takataka zote.
Hayo yamesemwa wakati wa ukaguzi wa viwanda hivyo na kubaini kuwa viwanda hivyo vipo ndani ya makazi ya watu, ambapo amesema serikali imewavumilia kutokana na udhaifu uliojitokeza kipindi cha nyuma.
Hayo yanajiri ikiwa ni wiki moja imepita tangu Mpanda Radio FM iripoti taarifa juu ya wananchi wa kata ya Mpanda Hotel kulalamikia viwanda vilivyopo eneo hilo na uchafu kutokutolewa kwa wakati na hivyo kusababisha kuibuka kwa ugonjwa wa mafua.
Kwa upande wake Mkurugenzi manispaa ya Mpanda Sophia Kumbuli amewataka wamiliki wa viwanda hivyo kuziondoa takataka zote na sio kuchoma kwani uchomaji unapelekea uchafuzi wa hali ya hewa.
Kwa upande wake Afisa Afya Manispaa ya Mpanda Erick Kisaka ametoa taarifa juu ya usafi wa kata ya Mpanda Hotel na Makanyagio ambapo amesema kuwa mashine zilizopo maeneo hayo zinazalisha taka nyingi ambazo zinasababisha uchafuzi wa mazingira na kupelekea manispaa kuwa chafu.
Wito umetolewa kwa wamiliki wa viwanda hivyo kuwa jambo hilo lisijirudie tena na endapo itabainika makosa hayo kujirudia serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria.