Wananchi Katavi hawana elimu ya utunzaji wa kinywa, meno
21 March 2024, 10:55 am
Picha na Mtandao
“Utafiti uliofanyika umegundua kuwa watoto wenye umri wa miaka sita hadi tisa ndio waathirika wakubwa“
Na Samwel Mbugi -Katavi
Wananchi Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wametoa maoni mseto kuhusiana na maadhimisho ya wiki ya afya ya kinywa na meno ambapo wameonesha kutokuwa na elimu ya kutosha ya namna ya utunzaji wa kinywa na meno.
Hayo yamebainishwa na wananchi wakati wakizungumza na Mpanda Radio Fm ambapo wamesema kuwa hawana elimu ya afya ya kinywa na meno ambapo wameitaka mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kila wakati bila kusubiri siku ya maadhimisho.
Kwa upande wake daktari anayehusika na afya ya kinywa na meno Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi Rhoda Mwakasege amesema kuwa utafiti uliofanyika wamegundua kuwa watoto wenye umri wa miaka sita hadi tisa ndio waathirika zaidi kwa kiasi kikubwa.
Pia amewataka wananchi kutokimbilia kutoa meno bila kufanya matibabu kwani kutoa meno inatakiwa kuwa hatua ya mwisho baada ya matibabu kushindikana.
Ikumbukwe kuwa kilele cha maadhimisho ya afya ya kinywa na meno kimefanyika tarehe 20 mwezi wa tatu mwaka huu, kwa kaulimbiu inayosema kinywa chenye furaha ni mwili wenye furaha.