Jamii FM

Dkt.Biteko akasirishwa na matumizi ya Milioni 759 ujenzi wa kituo cha Afya Msimbati

17 November 2024, 22:37 pm

Mwonekano wa kituo cha Afya Msimbati (Picha na Musa Mtepa)

Hii ni ziara ya kikazi ya Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati kutembelea katika mradi  wa ujenzi wa kituo cha Afya Msimbati ,ambao ni miongoni mwa miradi mitatu aliyoagiza mwaka 2023 alipofanya ziara mkoani Mtwara kwa Wananchi wa vijiji vya Msimbati,Mngoji na Madimba vjiji ambavyo gesi asili huzalishwa na kuchakatwa.

Na Musa Mtepa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, leo Novemba 17, 2024, amefanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa kituo cha afya kilichojengwa katika Kijiji na Kata ya Msimbati, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mkoani Mtwara.

Akiwa katika ukaguzi huo, Dkt. Biteko ameonesha kutoridhishwa na matumizi ya fedha za mradi huo, kiasi cha shilingi Milioni 759, zilizotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) huku akihitaji maelezo ya kutosha kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Abeid Abeid Kafunda, pamoja na Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo, Elius Kuyeko na hoji matumizi ya shilingi Milioni 159 ambazo ziliongezwa na TPDC baada ya kutolewa taarifa kwamba shilingi Milioni 600 zilizotengwa awali hazikutosheleza kugharamia ujenzi huo.

Sauti ya 1: Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amesema kwamba amefanya ziara kadhaa za ukaguzi wa mradi huo kupitia Kamati ya Usalama ya Mkoa. Akisema kamati hiyo ilikuwa na maswali mengi kuhusu thamani ya mradi, na alitoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia kwa karibu ili kubaini hali halisi ya kile kilichofanyika.

Aidha ameongeza kwamba, iwapo itabainika kuwa kuna kasoro zozote, hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Sauti ya Kanali Patrick Sawala, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Wakati huo, wananchi wa Kijiji cha Msimbati, wakiwemo Musa Ali na Athumani Mfaume Chande, wamepongeza jitihada za serikali za kujenga kituo hicho cha afya, wakisema kuwa kitatatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa akina mama,Wakielezea kuwa, kituo hicho kitawawezesha kupata huduma za uzazi kwa ukaribu na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali.


Sauti ya wananchi wa Kijiji na Kata ya Msimbati.