Jamii FM
Jamii FM
31/03/2026, 07:46

Wananchi wa Mnyahi, Mtwara, wailalamikia Shule ya Msingi Mnyahi kuwa na majengo chakavu, wanafunzi kunyeshewa darasani,Wadai imepuuzwa licha ya ufaulu mzuri, viongozi waahidi hatua za ukarabati
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kijiji cha Mnyahi, kata ya Milangominne Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara, wameiomba serikali kuangalia kwa jicho la tatu hali ya Shule ya Msingi Mnyahi kufuatia uchakavu wa majengo ya shule hiyo.Hali hiyo imeelezwa kusababisha wanafunzi kunyeshewa na mvua wakiwa darasani.
Wakizungumza na Jamii FM Radio Machi 28, 2026, wananchi hao wamesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo katika mitihani ya Darasa la Saba, bado haijapatiwa ukarabati wala ujenzi wa majengo mapya.
Aidha, wameeleza kuwa shule hiyo imejengwa mwaka 1973, na mara ya mwisho kupata majengo mapya ilikuwa wakati wa utawala wa hayati Rais Benjamin Mkapa.

Mkazi wa kijiji hicho, Abdulaaziz Bushiri Mjupa, amesema kutokana na serikali kutoipa kipaumbele shule hiyo katika ukarabati na ujenzi wa majengo, wananchi wamelazimika kuchangishana ili kupunguza baadhi ya changamoto, ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo hali ambayo ni tofauti na ilivyo katika shule za vijiji jirani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Salumu Mpangu, amekiri kuwepo kwa majengo yanayohitaji ukarabati mkubwa kutokana na uchakavu uliopitiliza.
Amesema tayari amewasilisha taarifa za hali hiyo katika vikao vya maendeleo ya kata zaidi ya mara tatu bila mafanikio yoyote.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri kufika kijijini hapo kujionea hali halisi na kuchukua hatua za haraka.
Naye Diwani wa Kata ya Milangominne, Mhe. Sharifu Kapela, amesema kata hiyo ina shule mbili zenye changamoto ya majengo chakavu zinazohitaji ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya.
Amezitaja shule hizo kuwa ni Milangominne na Mnyahi, akibainisha kuwa tayari ameshawasilisha suala hilo halmashauri na ameahidiwa kuwa litafanyiwa kazi kuanzia mwezi Agosti.
Pia ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia kuboresha miundombinu ya shule hizo.

Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Hassani Ali Mauji, amekiri kuwepo kwa shule chakavu katika halmashauri hiyo.
Amesema shule hiyo imeingizwa katika mpango wa BOOST unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka wa fedha wa serikali.
