TANECU yawaita Wananchi Katika Uzinduzi wa Kiwanda cha kubangua Korosho
30 September 2024, 11:27 am
Matarajio kwa miaka mitano ijayo katika uwekezaji wa viwanda vya korosho ni kuona wawekezaji kutoka nchini Uholanzi na china ambao wameonesha mahitaji ya korosho karanga.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Mtwara wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kiwanda cha kubangua korosho kilichojengwa katika Kijiji cha Mmovo, wilaya ya Newala.
Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba Newala Cooperative Union (TANECU), Ndug. Karim Chipola, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Chipola amesisitiza kwamba kiwanda hicho ni hatua muhimu ya ukombozi kwa wakulima wa korosho, kwani kitasaidia kuongeza thamani ya mazao yao.
Katika taarifa yake, Chipola amewaomba pia viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuungana katika uzinduzi huo, akitaja umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa vyama hivyo.
Akizungumzia changamoto za viwanda vya kubangua korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Ndug. Frances Alfred, ameeleza mikakati inayotekelezwa katika kuhakikisha viwanda vinavyosimamiwa na vyama vya ushirika vinapata mitaji kwa bei nafuu kupitia Benki ya Kilimo ili kusaidia kuzuia kufa kwa viwanda hivyo.
Frances Alfred pia amefafanua kwamba viwanda vingi vilivyoanzishwa hivi karibuni vinamilikiwa na wawekezaji wa ndani, huku akielezea matarajio ya kuja kwa wawekezaji kutoka Uholanzi na China katika miaka mitano ijayo.
Uzinduzi huu unatarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi wa wakulima na jamii kwa ujumla, hivyo wananchi wanashauriwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo.