TARI Naliendele yajizatiti kutoa elimu ya kilimo Msangamkuu Beach Festival
29 December 2024, 22:03 pm
Msangamkuu Beach Festival msimu wa nne umekuwa wa kipekee na hii ni kutokana na uwepo wa mabanda ya taasisi mbalimbali inayotoa elimu kwa wananchi juu ya huduma zinazotolewa na taasisi husika.
Na Musa Mtepa
Kituo cha Utafiti na Kilimo TARI-Naliendele kimewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Msangamkuu Beach Festival, na kutembelea banda la taasisi hiyo ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu kilimo na uongezaji wa thamani katika zao la korosho.
Akizungumza na Radio Jamii FM leo, Disemba 29, 2024, Festo Masisila, mtafiti kutoka TARI-Naliendele, amesema kwamba pamoja na kusherehekea tamasha hili, wananchi wanayo nafasi muhimu ya kutembelea banda la utafiti wa kilimo, kujifunza na kuuliza maswali kuhusu kilimo na jinsi ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Masisila amebainisha kuwa elimu inayotolewa inahusu mbegu bora, agronomia, na vithibiti vya magonjwa mbalimbali ya mazao.
Aidha, Baraka Zebedayo kutoka idara ya uongezaji thamani ya zao la korosho TARI-Naliendele, ameelezea matarajio ya kuendelea kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuongeza thamani ya korosho na ufahamu wa masoko ya bidhaa zinazotokana na korosho na bibo katika msimu huu wa Msangamkuu Beach Festival.
Wananchi waliotembelea banda la TARI-Naliendele wameonesha kuridhika na elimu waliyoipata, na kutoa wito kwa wengine kujitokeza ili kujifunza zaidi kuhusu kilimo na uongezaji thamani mazao.
Tamasha la Msangamkuu Beach Festival limefunguliwa rasmi tarehe 28 Disemba 2024 na linatarajiwa kuhitimishwa Januari Mosi, 2025 ambapo Katika kipindi cha tamasha hili wananchi watapata burudani za ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, na michezo ya ufukweni, pamoja na elimu mbalimbali zinazotolewa kwa jamii.