Kidato cha nne Manispaa ya Mtwara Mikindani wahimizwa kujiandaa na kesho iliyo bora
28 January 2025, 06:40 am
Hili ni kongamano lililohusisha shule ishiri za sekondari za serikali na binafsi zinazopatikana katika Manispaa ya Mtwara Mikindani lenye lengo la kuhamasisha wanafunzi na walimu kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa kuwa dhamira ya kuondoa ziro.
Na Musa Mtepa
Wanafunzi wa Kidato cha Nne kutoka shule ishirini za sekondari zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wameaswa kuongeza bidii katika masomo yao ili kujiandaa na kesho iliyo bora.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, wakati wa kongamano la elimu lililofanyika Januari 27, 2025, katika viwanja vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Kanali Sawala amesisitiza kuwa wanafunzi wanayo nafasi ya kujirekebisha, hasa wale waliowahi kufanya makosa katika kipindi cha nyuma, akisema kuwa elimu ya Kidato cha Nne ni muhimu kwa ajili ya kujenga mustakabali wao
Katika hotuba yake, Kanali Sawala pia amekumbusha wanafunzi wa kike kuepuka shinikizo la kuozeshwa kwa sababu ya kushindwa mitihani hivyo ni wakati wa kusoma kwa bidii kwani wanafunzi wa kike wanaweza kufikia nafasi mbalimbali za kitaaluma na kiutendaji.
Kanali Sawala ametoa pongezi kwa walimu wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa juhudi zao za kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo yao huku akiwasisitiza kuwa licha ya changamoto zinazozikabili , walimu wanapaswa kuendelea na kazi hiyo muhimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafanikio.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu tawala, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Mtwara, Mwalimu Dadi Ngahalo, ametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa mikakati inayotekelezwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mafanikio kwenye mitihani ya Kidato cha Nne.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassani Nyange, amesema kuwa halmashauri imeweza kufanikisha matokeo mazuri katika mitihani iliyopita na kwamba wanajitahidi kuondoa kiwango cha sifuri (zero) katika mitihani na kufikia nafasi za juu kitaifa.
Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria kongamano hilo wameeleza ahadi yao ya kujitahidi kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya Kidato cha Nne na kueleza kuwa kongamano hili limewapa motisha na kuomba makongamano kama haya yaendelee ili kuwapa msaada zaidi katika safari yao ya kielimu.