Jamii FM
Jamii FM
26 January 2026, 11:17 am

Jamii Mtwara imehimizwa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, kuimarisha makuzi yao, huku wadau wakitathmini huduma za malezi na kupanga mipango kupitia PJT-MMMAM.
Na Musa Mtepa
Jamii mkoani Mtwara imetakiwa kuhakikisha watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kuchanganya na chakula au kinywaji kingine chochote, ili waweze kupata makuzi sahihi.
Wito huo umetolewa January 23,2026 wakati wa kikao cha robo mwaka cha wadau mbalimbali wakiwemo asasi za kiraia kilicholenga kufanya tathmini ya shughuli zilizotekelezwa kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, pamoja na kupanga mipango kazi ya Januari hadi Machi 2026 kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za TCCIA mjini Mtwara.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja Mradi kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya KIMAS yenye makao makuu yake wilayani Masasi mkoani Mtwara, Torai Kibiti, amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya maeneo, ikiwemo uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na kitu kingine.
Amesema changamoto hiyo inatokana na imani potofu iliyopo katika jamii kwamba mtoto ambaye hajafikisha miezi sita hawezi kunyonya maziwa ya mama pekee, hali inayohitaji kuongeza juhudi za uelimishaji na hamasa kwa jamii.
Akiwasilisha mada kuhusu chombo cha kupima hali ya utekelezaji na ubora wa utoaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (Scorecard), kwa niaba ya Ofisa Ustawi wa Mkoa wa Mtwara, Ofisa Ustawi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Godlove Miho, amesema chombo hicho kinasaidia wadau kujitathmini na kubaini ubora wa huduma wanazotoa kwa watoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vituo vya Kulelea Watoto mkoani Mtwara, Selemani Issa Mkonga, amesema ili kufikia malengo ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, jamii haina budi kuwekeza katika uanzishaji wa vituo vya kulelea watoto, kwani idadi iliyopo kwa sasa haitoshelezi mahitaji.

Aidha, Issa Mkonga amesema upungufu au kukosekana kwa vituo vya kulelea watoto kumesababisha watoto wengi kukumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo unyanyasaji na vitendo vya ukatili mitaani, na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kuanzisha vituo hivyo kwa maslahi ya watoto.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM)inalengakuhakikisha watoto wote kuanzia mimba hadi umri wa miaka 8 wanapata malezi, makuzi na huduma bora ili wakuekimwili, kiakili, kihisia na kijamii , ikiwemo Afya na Lishe, Malezi Chanya na Ulinzi wa Mtoto, Elimu ya Awali na Maendeleo ya Akili, Makuzi ya Kihisia na Kijamii na Huduma kwa Watoto Wenye Mahitaji Maalum.