Wananchi wa Mtwara Mikindani wafurahia Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia
25 January 2025, 23:58 pm
Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia inatarajia kufanyika katika kipindi cha siku kumi katika mkoa wa Mtwara kwa kuanzia January 24,2025 hadi February 2,2024 ambapo uzinduzi wake umefanyika katika viwanja vya mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani
Na Musa Mtepa
Baadhi ya Wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wameonesha kufurahia kampeni ya msaada wa kisheria ilizinduliwa jana, Januari 24, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, katika Viwanja vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Wananchi hao wamesema kupitia kampeni hiyo, watapata msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali, ikiwemo ndoa, mirathi, umiliki wa ardhi, na mahusiano.
Akizungumzia kampeni hiyo, Bi. Rehema Aidani, mkazi wa Kata ya Mitengo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kuhudhuria viwanja hivyo ili kukutana na wataalamu wa sheria na kujifunza masuala ya kisheria ambayo yataweza kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande mwingine, Maulidi Samri Ahmad, mkazi wa Kata ya Mitengo, amesema kuwa atatumia fursa hiyo kuelezea changamoto zinazowakabili wakazi wa kata hiyo, hususan matatizo ya ardhi, kwani kumekuwepo na baadhi ya viongozi wanaojihusisha na ubadhirifu wa maeneo kwa kisingizio cha uwekezaji.
Mzee Saidi Ausi, mkazi wa Kata ya Mitengo, amesema kuwa yeye pia atatumia kampeni hiyo kupata wataalamu wa sheria kwa ajili ya kutatua changamoto ya ardhi inayomkabili. kwani yeye binafsi ameambiwa kuhama katika eneo aliloishi kwa miaka mingi, na amekutana na changamoto ya kutokuelewa vizuri uhalali wa madai hayo.
Katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Kanali Patrick Sawala, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amewasihi wananchi kuchangamkia fursa ya kupata ushauri wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu, migogoro ya ardhi, mirathi, na changamoto nyingine za kisheria.
Kampeni hii imeonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Mtwara Mikindani, ikitoa fursa ya kujua haki zao kisheria na kupata msaada wa kisheria kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.