Jamii FM

TARURA Mtwara yaianza miradi ya TACTIC ya bilioni 27.4

23 December 2025, 12:50 pm

Maandalizi ya ujenzi wa ofisi za TARURA na Maabara ya kupimia vifaa na miradi ya ujenzi wilaya ya Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

TARURA Wilaya ya Mtwara imeanza utekelezaji wa miradi ya TACTIC ikihusisha ujenzi wa ofisi, maabara ya kupima ubora wa miradi, barabara na mifereji ya maji, huku ikilenga kuboresha miundombinu na kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo

Na Musa Mtepa

TARURA Wilaya ya Mtwara imeanza utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) inayofadhiliwa na Serikali Kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, kwa kuanza ujenzi wa jengo la ofisi ya usimamizi wa miradi pamoja na maabara ya kupima ubora wa vifaa vya ujenzi na miradi.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 22, 2025 katika eneo la mradi, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Hatibu Nunu, amesema mradi huo unagharimu shilingi bilioni 27.4 na unatekelezwa na Mkandarasi Serengeti Limited. Amesema ujenzi huo umeanza rasmi Desemba 5, 2025 na utahusisha ujenzi wa ofisi tatu pamoja na chumba maalumu cha Maabara.

SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara

Mhandisi Nunu ameongeza kuwa miradi ya TACTIC pia inahusisha ujenzi wa Barabara ya Pacha ya Mbae yenye urefu wa kilomita 2.4, Barabara ya stendi ya Chipuputa yenye urefu wa kilomita 2.4, Barabara ya kuzunguka soko la Chuno yenye urefu wa kilomita 3 pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua.

SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara

Kwa upande wa ukarabati wa Barabara, amesema Wilaya ya Mtwara hutengewa shilingi bilioni 7 kwa mwaka kwa ajili ya halmashauri tatu, ambapo Manispaa ya Mtwara Mikindani hupata shilingi bilioni 3.8. Kwa mwaka huu, TARURA imesaini mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ukarabati wa Barabara na usafishaji wa mifereji, kazi ambazo tayari zinaendelea.

SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara

Naye Mhandisi Mshauri Mkazi wa miradi ya TACTIC katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Henry Moshi, amesema mkandarasi yupo katika hatua za maandalizi ya kazi (mobilization) na ameahidi kuwa vibarua wazawa watapewa kipaumbele katika ajira.

SAUTI: Mhandisi Henry Moshi – Mshauri wa Miradi ya TACTIC

Nao wananchi wakiwemo vijana na mama lishe wameeleza kufarijika na uwepo wa miradi hiyo wakisema italeta tija, kuongeza kipato na kuboresha mazingira ya biashara, huku wakiwahimiza vijana kutumia fursa zinazojitokeza.

SAUTI: Vijana na Mama Lishe