

23 March 2025, 15:39 pm
Haya ni maadhimisho ya 75 tangu kuanzishwa kwa shirika la hali ya hewa Duniani mnamo March 23 ,1950 ambapo Tanzania ikiwa nchi mwanachama 193 wa WMO na kwa Mtwara mjini yameadhimishwa katika chuo cha kilimo cha MATI Naliendele Mtwara.
Na Musa Mtepa
Wananchi mkoani Mtwara wameaswa kusikiliza kwa umakini tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha na kusaidia jamii kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga ya hali ya hewa.
Wito huo umetolewa leo March 23, 2025 na Renatus Kapenda, Afisa mfawidhi kituo cha hali ya hewa (TMA) – kilimo Naliendele, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani yaliyofanyika katika Chuo cha Kilimo cha Naliendele (MATI) mkoani Mtwara
Aidha amesema Jamii isipofuatilia utabiri wa hali ya hewa kuna uwezekano wa kufanya kazi kubwa za kilimo kwa kutojua mbele kuna nini na mwisho wa siku kutokupata mavuno aliyoyatarajia.
Kapenda ametoa ufafanuzi juu ya utabiri wa hali ya hewa unaotolewa kila siku kutoka kwa TMA unaohusiana na mvua zinazotarajia kunyesha katika baadhi ya maeneo huku hali ikiwa tofauti na uhalisia wa maeneo mengine na kusababisha jamii kuwa na wasiwasi taarifa hizo.
Mwalimu Juma Jafari, Mratibu wa Mtandao wa Vijana Tanzania (TK Movement) kwa Mtwara mjini, ametoa shukrani kwa TMA kwa kuadhimisha siku ya hali ya hewa Duniani, akisema kwamba hii itasaidia vijana kutambua majanga yanayoweza kutokea na namna ya kuyakabiliana nayo kwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa.
Kwa upande wa wanafunzi wa Chuo cha Kilimo Naliendele (MATI) Mtwara, wameelezea furaha yao kwa kushiriki katika maadhimisho hayo, wakisema kuwa yameongeza uelewa wao kuhusu uhusiano wa hali ya hewa na shughuli za kilimo huku wakiahidi kutumia maarifa hayo katika kazi zao za kilimo baada ya kumaliza masomo yao.