Jamii FM

Shirika la ADEA laanza na mafunzo ya uchongaji kwa Wasanii Mtwara

16 November 2024, 14:01 pm

Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na afisa utamaduni na michezo Bi Ursula Kayombo baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo(Picha na Musa Mtepa)

Haya ni mafunzo yanayohusisha katika fani kuu nne ambazo ni uchoraji,uchongaji,ufundi seremala na ufundi chuma  ambapo kwa hatua ya awali wameanza na sanaa ya uchongaji.

Na Musa Mtepa

Novemba 15, 2024, Shirika linalojihusisha na sanaa na utamaduni mkoani Mtwara, ADEA, limeanza kutoa mafunzo kwa kundi la kwanza la wasanii wa uchongaji.

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Kuimarisha Sanaa, Utamaduni na Ufundi Stadi kwa Vijana, yanayofadhiliwa na UNESCO na Alwaleed Philanthropies.

Akifungua mafunzo hayo, Bi. Ursula Kayombo, Afisa Utamaduni na Michezo wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, amelipongeza shirika la ADEA kwa juhudi zake za kuwakutanisha wasanii wa uchongaji na kuwapatia elimu ya sanaa kwa pamoja na  matumaini yake kuwa, baada ya mafunzo, wasanii hao wataweza kutengeneza bidhaa bora zinazoweza kuvutia soko la ndani na nje ya nchi.

Sauti ya 1 Ursula Kayombo afisa utamaduni na michezo Manispaa ya Mtwara Mikindani
Afisa utamaduni na michezo Manispaa ya Mtwara Mikindani Ursula Kayombo akizungumza na washiriki wa Mafunzo (Picha na Musa Mtepa)

Kayombo amesisitiza umuhimu wa wasanii kutumia ujuzi watakaoupata katika mafunzo hayo kutengeneza bidhaa za ubora, ambazo zitawawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Sauti ya 2 Ursula Kayombo afisa utamaduni na michezo Manispaa ya Mtwara Mikindani

Saidi Chilumba, Mkurugenzi Mtendaji wa ADEA, amesema kuwa mafunzo haya yameanza na kundi la vijana saba kutoka maeneo mbalimbali ya Mtwara.

Aidha Chilumbaamesema kuwa shirika linakusudia kuwapatia wasanii hao ujuzi na misingi bora ya uchongaji, ili kuwasaidia kujenga soko la ndani na la kimataifa.

Sauti ya Saidi Chilumba mkurugenzi wa ADEA

Kwa upande mwingine, Mwezeshaji wa mafunzo, Thiago Mtanda, amesema kuwa mafunzo hayo yatazingatia vipimo na ubora wa bidhaa katika utengenezaji wa sanaa ya uchongaji, huku lengo kuu likiwa ni kusaidia wasanii hao kufahamu zaidi kuhusu soko la kimataifa.

Sauti ya Thiago Mtanda mwezeshaji wa mafunzo ya wasanii wa sanaa ya uchongaji

Wasanii wawili wa uchongaji, James Matupa na Paulina Frank, walieleza matumaini yao kuwa mafunzo haya yatawasaidia kutengeneza bidhaa bora zitakazowapa fursa ya kupata soko la uhakika, tofauti na hali walivyokuwa kabla ya kuanza mafunzo hayo.

Sauti ya wasanii wa sanaa ya Uchongaji mkoani Mtwara

Mafunzo hayo yanafanyika katika ofisi za ADEA, zilizopo mtaa wa Sinani, Manispaa ya Mtwara Mikindani, katika ofisi zilizo na makumbusho ya utamaduni wa makabila makuu ya Mkoa wa Mtwara, yaani Makonde, Makua na Yao (MAKUYA). Hii ni sehemu ya kundi la kwanza katika mafunzo hayo, ambayo yatadumu kwa miezi miwili.